……………………..
Na.Alex Sonna,Chamwino
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo,amesema kuwa Serikali inatarajia kutoa jumla ya Sh bilioni 33.5 kwa ajili ya kujenga wodi katika hospitali 67 Mpya za wilaya zinaoendelea kujengwa nchini kote.
Waziri Jafo ameyasema leo wakati wa ziara ya kukagua ujenzi hospitali ya Wilaya ya Chamwino inayojengwa kijiji cha Mlowa Barabarani iliyopo jijini Dodoma
Waziri Jafo amesema kuwa Rais John Magufuli ametoa shilingi milioni 500 kwa kila hospitali za wilaya zilizojengwa ili zitumike kujenga wodi za kulaza wagonjwa.
Mhe.Jafo amefafanua kuwa fedha hizo hatazitoa mpaka mnihakikishie kuwa ujenzi wa majengo saba yanakamilika kwa asilimia 100, najua endapo fedha zitatolewa mapema watu wanaweza ‘kuhamisha goli’ (kuzitumia kwa matumizi mengine).
”Mkishamaliza majengo ya awali kwa asilimia 100 fedha hizo nitawapa”Waziri Jafo
Aidha Mhe.Jafo amesema kuwa ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Chamwino na kutaka umaliziaji ukamiliki kwa wakati.
” Naona mlipofika nimeridhishwa na hatua hii japo kuwa mmechelewa, hali ambayo mlikuwa nayo awali ilikuwa mbaya hivyo viongozi tusingesimamia kwa karibu mpaka sasa kungekuwa hakuna kitu.” Amesema Mhe.Jafo
Mhe.Jafo amemtaka Mhadisi mshauri kuhakikisha kuwaa anasisimami kwa karibu umaliziaji uliobaki ili kusiwe na kasoro ambazo zinaweza kuharibu kazi nzuri iliyofanyika.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Chamwino, Athuman Masasi amesema kuwa walipokea Sh bilioni 1.5 na kutumia Sh bilioni 1.438 tangu kuanza ujenzi huo Februari mwaka huu na kubakiwa na Sh milioni 61.
” Ujenzi wa majengo haya umefikia zaidi ya asilimia 80 na tuko katika hatua za umaliziaji”amesema Masasi
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ametoa pongezi kwa Serikali na kuihakikishia kuwa huduma za afya zinaimarika katika mkoa wa Dodoma, huku pia akisema kuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linatarajia kuingiza umeme katika majengo hayo kuanzia wiki ijayo.
” Mkandarasi aliyepewa kazi ya kufikisha umeme wa REA ndiye atakayeingiza umeme kwenye majengo yetu haya na kazi hii inaanza wiki ijayo.”amesisitiza Dk.Mahenge