Home Mchanganyiko EfG YATOA SEMINA KWA WAFANYABIASHARA WANAWAKE MASOKONI KUHUSU SHERIA YA HUDUMA NDOGO...

EfG YATOA SEMINA KWA WAFANYABIASHARA WANAWAKE MASOKONI KUHUSU SHERIA YA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA

0
 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Equality for Growth (EfG), Jane Magigita,akichangia mada katika semina iliyohusu Sheria ya huduma ndogo za fedha iliyotolewa kwa wanawake wafanyabiashara masokoni jijini Dar es Salaam juzi.
 Mwezeshaji a Semina hiyo,  Emmanuel Joseph akitoa mada.
 Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake wafanyabiashara katika Soko la Mchikichini, Adela  Swai,  akichangia jambo kwenye semina hiyo.
  Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake wafanyabiashara katika Soko la Ilala, Consolatha Cleophas   akichangia jambo kwenye semina hiyo. 
 Ofisa Miradi wa EfG,Susan Sitta akizungumza.
 Majadiliano ya vikundi yakifanyika.
 Majadiliano ya vikundi yakifanyika.

 

Na Dotto Mwaibale
 
SHIRIKA lisilokuwa la kiselikari la Equality for Growth (EfG) linalopinga ukatili wa kijinsia kwa wafanyabiashara wanawake masokoni, limeendesha semina kwa wanawake hao ya kuwapa uelewa wa sheria ya huduma ndogo ya fedha, 2019.
 
Akizungumza na vikundi vya wafanyabiashara wanawake kutoka masoko 16 ya jijini Dar es Salaam juzi, Mwezeshaji wa semina hiyo, Emmanuel Joseph alisema mtu yeyote au kikundi kinaweza kusajiliwa kwa kufuata taratibu zilizoainishwa katika sheria ya huduma za fedha za mwaka 2018.
 
“Kikundi cha kijamii kinachotarajia kutoa huduma ndogo za fedha kitatakiwa kufanya maombi ya usajili katika ngazi ya serikali za mitaa kwa kujaza fomu maalumu,” alisema Joseph.
 
Alisema maana ya huduma ndogo za fedha ni huduma zinazotolewa na mtu au taasisi za fedha ikiwemo kutoa na kuzipokea kwa njia mbalimbali kama vile mikopo na kuzihifadhi.
 
Joseph alizitaja huduma zinazoruhusiwa kutolewa na kikundi cha huduma ndogo za fedha kuwa ni kutoa hisa za uanachama, kuhamasisha akiba kutoka kwa wanachama wake,kutoa mikopo, kuhamasisha hisa za wanachama na kununua hisa katika masoko salama.
 
Alitaja adhabu zinazoweza kuchukuliwa kwa atakayekwenda kinyume cha matakwa ya sheria na kukutwa na hatia kuwa atalipa faini isiyo chini ya sh. milioni tano na isiyozidi milioni ishirini au kifungo kisicho chini ya miezi mitatu au kisichozidi miaka mitano au vyote.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa EfG, Jane Magigita alisema wameupokea mswada huo ndiyo maana wameamua kutoa semima ya uelewa kwa vikundi hivyo vya wafanyabiashara wanawake sokoni.
 
Magigita alisema wanawake wanaofanya biashara sokoni wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa lakini viongozi wa serikali wamekuwa hawawaungi mkono.
 
“Tunawaomba viongozi wa serikali kuanzia maafisa watendani, madiwani, wabunge, wakuu wa wilaya na wale wa ngazi ya juu  wawatembelee wanawake wanaofanya biashara sokoni kujua changamoto zinazowakabili kwa sababu wanamchango mkubwa katika taifa letu,” alisema.
 
Alisema tangu shirika hilo lilipoanzisha vikundi na kuwapa elimu ya uelewa wa haki zao na kupinga vitendo vya kikatili na unyanyasaji dhidi ya akina mama sokoni, kiongozi pekee wa ngazi ya juu aliyewahi kutembelea Soko la Buguruni ni alikuwa Makamu wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Gharibu Billal.
 
Mwenyekiti wa Kikundi cha akina mama wanaofanyabiashara katika Soko la Kisutu, Shamsia  Ulimwengu aliipongeza EfG kwa kuwapa uelewa wa kuzitambua haki zao tofauti na zamani walipokuwa wakikumbana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na kukosa msaada.
 
 
Vikundi vilivyohudhuria semina hiyo ni kutoka masoko ya Mbagala, Gongo la Mboto, Kinyerezi, Ilala, Mchikichini, Buguruni, Feri,Kisutu, Kigogo Fresh, Kigogo Sambusa, Kiwalani, Gezaulole, Mombasa,Temeke Stereo, Kampochea na Tabata Muslim.
 
Hivi karibuni serikali ilitoa mswada kuhusiana na usajili wa vikundi kulingana na Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha za Mwaka 2019 ambapo wahusika wanaujadili ili kupata maoni kabla ya kutoka kanuni.