NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MKOA wa Pwani, kwa mara ya pili unatarajia kufanya maonyesho ya viwanda kuanzia tarehe 1-7 octoba mwaka huu, huku ukitarajia kuongeza idadi ya wawekezaji watakaoshiriki kutoka 166 mwaka 2018 hadi kufikia 500.
Maonyesho hayo yataambatana na kongamano la uwekezaji litakalofanyika octoba 3 ambapo yatafanyika katika uwanja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),maarufu uwanja wa sabasaba uliopo ,Mkuza wilayani Kibaha mkoani hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo na kusainishana mkataba baina ya mkoa na waratibu hao, mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema, waratibu wa maonyesho hayo watakuwa ni wabobezi wa masuala ya maonyesho kama hayo kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) pamoja na mamlaka ya maendeleo ya viwanda (TANTRADE) .
Alieleza, malengo ya matukio hayo ni kuonyesha kwamba mkoa wa Pwani ,umedhamiria kuwa ukanda wa viwanda,wenye viwanda kupata masoko ya uhakika,kupanua wigo wa soko la ndani ya mkoa kufikia kimataifa na ,kuvutia wawekezaji wapya.
Aidha Ndikilo alifafanua lengo la kongamano hilo ,kuwa ni kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo utalii,uchumi,kijamii,kilimo,uvuvi na viwanda.
“Kufanyika kwa kongamano hili italeta picha halisi ya fursa zote zilizopo mkoani Pwani,na kuonyesha namna mkoa ulivyopiga hatua katika sekta ya viwanda,uwekezaji na fursa za miradi mikubwa ikiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa uzalishaji umeme megawatts 2,100 STIGO ,huko Rufiji”alibainisha Ndikilo.
Hata hivyo,mkuu huyo wa mkoa alisema wenye viwanda maonyesho ya mwaka jana walikuwa 166 mwaka huu wanatarajia kufikia 500 japo sio namba sahihi,na idadi ya watu watakaotembelea kuongezeka kutoka 18,000 hadi kufikia 100,000.
Nae Januarius Maganga wa TSN alisema ,wanakwenda kuratibu maonyesho hayo ikiwa ni maonyesho ya kumi .
Kwa upande wake ,mwakilishi wa mkurugenzi kutoka TANTRADE ,Victor Rugemalila aliwahakikishia wananchi na mkoa kwamba ,wamejipanga kuona namna bidhaa inakua na kuleta maendeleo ya wenye viwanda na kuratibu kwa ufanisi mkubwa maonyesho hayo.