Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima akikagua sehemu ya kutolea dawa katika kituo cha Afya cha Rudi wakati alipotembelea vituo vya kutolea huduma kwa lengo la kujionea maendeleo ya utoaji wa huduma za afya kwa jamii pamoja na matayarisho ya vituo hivyo katika kushiriki huduma za afya ya kinga Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima akitoa maelekezo kwa watumishi wa kituo cha Afya Kibakwe wakati alipotembelea vituo vya kutolea huduma kwa lengo la kujionea maendeleo ya utoaji wa huduma za afya kwa jamii pamoja na matayarisho ya vituo hivyo katika kushiriki huduma za afya ya kinga Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma
- Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima akikagua vitanda katika kituo cha Afya cha Rudi wakati alipotembelea vituo vya kutolea huduma kwa lengo la kujionea maendeleo ya utoaji wa huduma za afya kwa jamii pamoja na matayarisho ya vituo hivyo katika kushiriki huduma za afya ya kinga Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma
…………………………………………
Na. Angela Msimbira MPWAMPWA
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Dkt Archard Rwezahura amesema kituo cha Afya cha Kibakwe kimeteuliwa kuwa cha mfano wa utekelezaji wa mabadiliko katika utoaji wa huduma bora kwa jamii na kuwa Kituo Darasa kama ilivyofanyika kwenye Kituo cha Afya cha Makole kilichopo Manispaa ya Dodoma.
Ameyasema hayo wakati akiwa kwenye ziara iliyoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipotembelea vituo vya kutolea huduma Halmashauri ya Mpwapwa kwa lengo la kujionea maendeleo ya utoaji wa huduma za afya kwa jamii pamoja na matayarisho ya vituo hivyo katika kutoa huduma za afya kinga.
Dkt, Rwezahura amesema uamuzi huo umefikiwa kulingana na fursa kubwa zilizopo sasa katika kituo hicho ukilinganisha na awali hususani maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano.
Amesema kuwa, Kituo cha Afya cha Kibakwe ni kituo ambacho kimefanyiwa marekebisho makubwa ya miundombinu ikiwemo majengo ya upasuaji, wodi ya mama na mtoto, maabara, chumba cha kuhifadhia maiti hivyo, fursa kubwa ya kuvutia wateja kwa kuinua uwajibikaji wa watumishi ili maboresho hayo ya wanufaishe wateja na serikali kwa ujumla.
Dkt. Rwezahura ametaja baadhi ya vigezo ambavyo wamevitumia katika kuteua kituo hicho kuwa cha mfano wa maboresho ya uwajibikaji unaopimika kuwa ni pamoja na uwepo wa miundombinu bora, uwepo wa watumishi wenye sifa, kituo kuwa karibu na kufikika kwa urahisi, uwepo wa dawa na vifaa tiba vinavyohitajika na uwezekano wa kufanya ufuatiliaji wezeshi kwa urahisi.
Ameendelea kufafanua kuwa kwa mazingira haya, inawezekana kuiga mfano wa Kituo cha Afya Makole katika Manispaa ya Dodoma kilichofanikiwa kuinua uwajibikaji wake kwa siku 90 tu na mabadiliko makubwa yakaonekana ikiwemo kupanua wigo wa huduma, kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma na kukua kwa mapato ya uchangiaji mara mbili ukilinganisha na awali.
Wakati huohuo Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima amewataka watumishi wa kituo hicho kuleta mabadiliko ya uwajibikaji kutoka utendaji wa mazoea kwenda uwajibikaji unaopimika wazi.
“Mwelekeo wa OR -TAMISEMI ni kuwa na vituo bora vya afya ambavyo watumishi wake wanawajibika kwa mwelekeo mpya unaopimika kwa kadri ya rasilimali walizonazo ili, utoaji wa huduma uwe bora na kuvutia wananchi kujiunga na bima ya afya hususani CHF iliyoboreshwa ili kuimarisha uchumi wa sekta ya afya na kupunguza utegemezi kwa serikali kuu” Amesisitiza Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima anafafanua kuwa, dhamira ya serikali ni kuwa na watumishi wenye kufanya kazi kwa ubunifu na kuvithamini vituo hivyo kama wanavyothamini mali zao, kwa kuweka mikakati ya uwajibikaji wenye kupimika kuanzia mtumishi mmoja mmoja hadi timu nzima kama ilivyowezekana kwenye Kituo cha Afya Makole.
Amesema mikakati shirikishi itakayosimamiwa na wataalamu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa itachochea na kuchochea kasi ya kuboresha huduma, kuvutia wananchi kujiunga na bima ya afya na kuwa na nguvu ya kiuchumi kwa maendeleo ya sekta ya afya,
“Tunataka vituo vyote vya kutolea huduma nchini viwe na nguvu ya kiuchumi siyo kwa kutegemea watu waugue bali wananchi wenye afya bora wanaothamini kuchangia bima ya afya ili, pale wanapohitaji huduma wazipate zilizo bora, kwa gharama nafuu tena karibu na makazi yao hivyo, tuwekekeze kwenye uwajibikaji wenye mwelekeo mpya unaopimika hususani, huduma bora kwa mteja”. Amesema Dkt. Gwajima
Aidha Dkt. Gwajima ametoa siku 90 kwa kituo hicho pamoja na vituo vingine vyote nchini kama ilivyoazimiwa kwenye mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kubadili mwelekeo wa kufanya kazi kwa uwajibikaji unaopimwa kama wanavyofanya Kituo cha Afya Makole.
Naye Mganga Mkuu wa Kituo hicho Dkt. Pius Mramba pamoja na watumishi wote walipokea agizo hilo na kuahidi kutambua fursa zilizopo na kuahidi kuwa, watahakikisha wanakwenda na kasi hiyo na wako tayari kuingia kwenye ushindani wa ubora wa huduma na kupimwa.
Aidha, Vituo vilivyotembelewa ni pamoja na Kituo cha afya cha Kibakwe na Kituo cha afya Rudi kilichopo kilomita 100 toka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma.