Mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya rufaa ya Haydom ya Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, Dkt Emmanuel Nuwass (kushoto) akizungumza na madaktari wenzake.
Mkurugenzi wa tiba wa hospitalivya rufaa ya Haydom Dkt Emmanuel Nuwass akizungumza na madaktari wenzake wa hospitalini hapo baada ya kupokea mashine mpya ya mionzi ya CT Scan.
Mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya rufaa ya Haydom Mkoani Manyara, Dkt Emmanuel Nuwass akizungumza na waandishi wa habari, baada ya mashine mpya ya kisasa ya uchunguzi wa mionzi CT Scan kufikishwa hospitalini hapo.
*********************
HOSPITALI ya rufaa ya Kilutheri ya Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, imenunua mashine mpya ya kisasa ya uchunguzi ya mionzi (CT Scan) ambayo kwa miaka miwili hakukuwa na huduma hiyo baada ya iliyokuwepo awali kuharibika.
Hospitali hiyo kwa mwaka uhudumia zaidi ya wagonjwa 105,296 wa nje na 14,020 wa ndani wa mikoa sita ya Manyara, Arusha, Tabora, Singida, Dodoma na Simiyu.
Mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya Haydom Dk Emmanuel Nuwass alisema sh800 milioni zimetumika kuinunua Ujerumani na kuisafirisha mashine hiyo ya kisasa hadi hospitalini hapo.
Dk Nuwass alisema awali mashine waliyokuwa nayo iliharibika miaka miwili iliyopita hivyo kusababisha wagonjwa wengi kukosa huduma ya vipimo hivyo.
Alisema kutokana na ukosefu wa mashine hiyo iliwabidi watu wa eneo hilo kufuata vipimo hivyo takribani kilomita 400 hadi 600 kwenye hospitali za kanda za KCMC Kilimanjaro na Bugando Mwanza.
“Mashine hiyo ya kisasa itasaidia wagonjwa wengi hasa wasio na kipato kuweza kupata vipimo kwenye eneo la karibu na tunatarajia kumuomba Waziri wa Afya Ummy Mwalimu atuzindulie hivi karibuni,” alisema Dk Nuwass.
Mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo, Catherine Faustine alisema wananchi wengi wameshindwa kupata huduma hiyo kutokana na umbali mrefu wa kufuata katika hospitali nyingine kubwa.
“Kuna baadhi hata wamefariki kwa sababu hawana fedha za kwenda kupimwa katika hospitali za mbali ikiwemo KCMC Moshi au Muhimbili Dar es salaam, tunashukuru kwa kupata mashine hii,” alisema.
Mtaalamu wa mionzi wa hospitali hiyo Paul Fissoo alisema mashine hiyo mpya ina uwezo mkubwa zaidi tofauti na ile ya awali iliyoharibika.
Hospitali ya Kilutheri ya Haydom inayomilikiwa na KKKT Dayosisi ya Mbulu ilianzishwa na wamisionari wa Norway mwaka 1955 ikiwa na vitanda 50 na sasa ina vitanda 420.
Wagonjwa wanaopata huduma hospitali hiyo wanatoka wilaya za Mbulu, Hanang na Babati mkoani Manyara, Karatu mkoani Arusha, Igunga mkoani Tabora, Iramba na Mkalama mkoani Singida, Kondoa mkoani Dodoma na Meatu mkoani Simiyu.