Home Biashara Baadhi ya wananchi Wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameziomba taasisi mbalimbali za kifedha...

Baadhi ya wananchi Wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameziomba taasisi mbalimbali za kifedha kuongeza vituo vya kutolea huduma za kibenki

0

Baadhi ya wananchi Wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameziomba taasisi mbalimbali za kifedha kuongeza vituo vya kutolea huduma za kibenki katika maeneo ya vijijini ili kupunguza changamoto ya wafanyabiashara kuvamiwa na kuporwa fedha zao pale wanaposafiri na fedha kwenda kununua bidhaa
mbalimbali hasa nafaka.

Wakizungumza wakati wa mkutano wa biashara na wateja wa benki ya NMB wilayani Kasulu mkoani Kigoma, wananchi hao walisema kuwa kumekuwepo na matukio ya mara kwa mara ya wafanyabiashara kuvamiwa na kunyang’anywa fedha zao jambo walilodai kuwasababishia usumbufu na kushindwa
kufanya biashara kutokana na kuwepo kwa vitendo hivyo.

Bi.Emmakulatha Mazina ambaye ni mfanyabiashara wilayani humo alisema uwepo wa taasisi za kifedha katika maeneo ya vijijini itasaidia pia kuongeza mzunguko wa fedha na kukuza biashara hasa kutokana na baadhi ya wakulima na wanunuzi wa mazao wakifanya biashara kwa hofu ya kuvamiwa, huku pia wakiomba serikali na wadau wengine wa maendeleo kutoa elimu kwa wananchi wa vijijini juu ya namna bora ya kuhifadhi fedha kwenye mabenki ili kuepuka hasara zisizokuwa za lazima zinazoweza kujitokeza.

“Wafanyabiashara kusafiri na pesa kwa sasa ni hatari sana katika maeneo yetu, unakuta mtu anaenda kijijini kununua mahindi au mihogo na hata mazao mengine akiwa na pesa mikononi, majambazi wakijua tu anatafuta bidhaa wanaanza kupanga njama za kumvami”alisema.

Aidha wafanyabiashara hao waliipongeza benki ya NMB kwa kutoa huduma za kibenki katika maeneo mengi ya mkoa wa Kigoma na kuomba benki hiyo kuendelea kuboresha huduma kwa wateja wake pamoja na kuona haja ya kutoza viwango vya riba za mikopo kwa kuzingatia hali ya kipato cha maeneo
husika.

Pia waliiomba benki hiyo kuharakisha mchakato wa utoaji mikopo mikubwa kwa wateja kwa kuwaruhusu mameneja wa matawi kufanya tathimini na kumuidhinisha mteja kukopeshwa mkopo mkubwa tofauti na ilivyo sasa ambapo mteja hulazimika kusubiri majibu kutoka ngazi ya kanda na makao makuu ya ofisi za benki hiyo hali waliyosema imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwao.

Kwa pande wake Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi Sospeter Magesse alisema benki hiyo inaendelea kutatua changamoto zilizopo katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha malengo ya benki hiyo kuwahudumia wananchi yanafanikiwa kama ilivyokusudiwa.

Aidha alisema kuwa benki hiyo imeanza utaratibu wa kushusha madaraka ya kutoa mkopo hadi bilioni moja kwa mameneja wa benki ngazi ya tawi ili baada ya kupokea maoni kutoka kwa wateja wake katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tunajaribu kuweka mambo sawa yakiwemo ya kisheria ili kujaribu kulegeza vigezo na masharti, lakini pia tuna mikopo ya aina nyingi mfano unahitaji kukopa milioni sitini za kujenga kiwanda, hapo lazima taratibu zifanyike hata kuanzia ngazi ya chini hadi kwenye bodi yetu ya wakurugenzi na wao ndio wenye
mamlaka ya kuruhusu mkopo huo utolewe”alisema meneja huyo.

Awali akiwasilisha mada katika mkutano huo mshauri wa masuala ya kibiashara kutoka kampuni ya TRUEMAISHA TRAINING COMPANY Bwana Erick Chrispin ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni hiyo aliwapongeza wafanyabishara wa wilaya ya Kasulu kuwa na idadi kubwa ya wafanyabiashara wanaofanya vizuri katika biashara zao huku akiwashauri kuwa makini katika kufanya biashara kwa kutumia mbinu za kitaalamu ambazo zitawasaidia kuepuka kupata hasara na kuona biashara kama mzigo.