Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Innocent Bashungwaakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda litakalofanyika jijini Dar es salaam Septemba 6, 2019.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Innocent Bashungwa amesema Tanzania na Uganda zinatarajia kufanya Kongamano la Kibiashara la pamoja ikiwa ni mara ya Kwanza kufanyika nchini.
Bashungwa ameyasema hayo leo mbele ya Waandishi wa Habari ambapo amesema Kongamani hilo linatarajia kufanyika Septemba 6, 2019 kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
“Kongamano hili la kibiashara baina ya Tanzania na Uganda ambalo litawashirikisha wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda litasaidia kuweka mazingira wezeshi ya kuongeza wigo wa kujenga viwanda zaidi nchini hasa vya usindikaji wa mazao ili kuongeza thamani ya mazao hayo”
Mpaka sasa Tanzania inauza bidhaa za mazao na bidhaa za viwandani nchini Uganda ambapo takwimu zinaonesha kwa miaka miwili iliyopita Tanzania imeweza kuuza bidhaa za mazao ya chakula na viwandani zenye thamani ya shilingi Bilioni 300 kutoka Bilioni 100 ambalo ni ongezeko mara mbili ya fedha zilizopatikana huko nyuma.
Waziri Bashungwa amewakaribisha wafanyabiashara na wadau mbalimbali kujiandikisha ili kushiriki katika kongamano hilo ambalo litafungua fursa nyingi kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda, hivyo kuongeza fursa zaidi za kibiashara kati ya nchi hizo.