Mkuu wa Wilaya ya Kusini Idrisa Mustafa Kitwana akizungumza na Vijana wakati akifungua Kongamano la Vijana kuhusu fursa za kiuchumi visiwani Zanzibar huko katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Kikwajuni Zanzibar.
Mkurugenzi wa Masoko kutoka Kamisheni ya Utalii Dkt.Miraji Ussi akiwasilisha mada kuhusu Uchumi katika Sekta ya Utalii huko Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Kikwajuni Zanzibar katika Kongamano la Vijana .
Kombo Dhikiri Kombo kutoka chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) akiuliza maswali kuhusu mada ya Uchumi Sekta ya Utalii katika Kongamano la Vijana huko Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Kikwajuni Zanzibar
Picha ya pamoja akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kusini Idrisa Mustafa Kitwana wanne (kulia), Vijana na viongozi wengine kutoka Sekata mbali mbali.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
………………..
NA Mwashungi Tahir Maelezo
Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrissa Mustafa Kitwana amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo visiwani Zanzibar kwa lengo la kujitengenezea ajira na kuacha kusubiria ajira kutoka Serikalini.
Akizungumza hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud huko katika Ukumbi wa Idriss Abdul-Wakil wakati wa kufungua Kongamano la vijana kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo visiwani Zanzibar.
“ Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa katika kuinua uchumi nchini hivyo ni lazima mjikite katika kujituma wenyewe ili waweze kujipatia kipato cha halali,”alisema Mkuu wa Wilaya.
Amewataka vijana kizitumia fursa ziliopo katika kujiajiri wenyewe kwa kufanya kazi mbali mbali zenye kuwapatia rizki na kuacha kusubiria ajira kutoka Serikalini ikiwa Serikali haiwezi kuajiri vijana wote.
Aidha alisema ili vijana wawe na mustakabali mzuri wa kukuza uchumi ndani ya nchi na kujiendeleza maisha yao lazima wawe na elimu,wajiepushe na madawa ya kulevya ili Taifa liweze kuwa na vijana wenye afya bora na kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi .
“Elimu ndio ufunguo wa maisha hivyo itumieni elimu kwa kuifanyia kazi mbali mbali ikiwemo ujasiriamali kilimo na sio kuweka vyeti ndani na kusubiri ajira wakati unakupiteni”, alisema Idrissa.
Akitoa wito kwa vijana kuwataka kuhakikisha kongamano hilo litawajengea uwezo na wakitoka hapo waweze kubadilika kwa kuibua mambo mengi katika kujiongezea kipato chao.
Mh Idrissa amewataka vijana kuacha kufikiria kwamba utalii ni kutembeza wageni tu ila kuna kazi nyingi ambazo ni za utamaduni wetu ujasiriamali tukizifanya watalii watavutiwa nazo na pato litaingia nchini.
Nae Dkt Miraji Ussi Mkurugenzi Masoko Kamisheni ya Utalii amesema Zanzibar utalii unakuwa miradi mingi ipo ya kuvutia watalii ikiwemo spice, kusuka mikeka na mambo mengine vijana wafanye kazi hizo ili kukuza uchumi.
Pia amesema miradi mingine ni sekta ya malazi, bangaloo, na michezo ya ngoma za kiasili na mambo mengi ya Wazanzibar ambapo watalii huvutika nayo na kuwaomba vijana wachangamkie fursa hizo.
Wakitoa michango katika kongamano hilo Siti Hussein Jumamwanafunzi kutoka Skuli ya Benmbela aliiomba Kamisheni ya Utalii kuwapangia sera maalum watalii wanapoingia nchini kuhusu suala la kivazi ili utamaduni wetu wetu uweze kuimarika .
Kongamano hilo la siku moja mada nne ziliwasilishwa ikiwemo Ujasiriamali , Uchumi sekta ya utalii, uchumi wa visiwani,na uchumi mafuta na gesi na kauli mbiu ya Kongamano hilo “TUMIA ELIMU KUWA FURSA YA MAENDELEO YA KIUCHUMI”.