Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akimsikiliza
Mtangazi wa Kituo cha Channel Ten na Redio Magic, Nelson Munema,
alipokuwa anamuhoji kuhusu usalama wa nchi, ofisini kwa Waziri
huyo, jijini Dar es Salaam, leo. Katika mahojiano hayo, Lugola alitoa
onyo kali kwa vyama vya siasa nchini ambavyo vimetangaza kufanya
mikutano ya hadhara kabla ya muda uliopangwa kwa ajili ya uchaguzi
wa Serikali za Mitaa nchini unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na
waandishi wa Kituo cha Channel Ten na Redio Magic (hawapo
pichani), wakati walipokuwa wanamuhoji jijini Dar es Salaam, leo,
kuhusu hali ya usalama wa nchi. Katika mahojiano hayo, Lugola
alitoa onyo kali kwa vyama vya siasa nchini ambavyo vimetangaza
kufanya mikutano ya hadhara kabla ya muda uliopangwa kwa ajili ya
uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini unaotarajiwa kufanyika hivi
karibuni. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
******************
Na Felix Mwagara, MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametoa onyo kali kwa
vyama vya siasa nchini ambavyo vimetangaza kufanya mikutano ya
hadhara kabla ya muda uliopangwa kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za
Mitaa nchini.
Waziri Lugola ameyasema hayo wakati alipokuwa katika mahojiano
maalum na chombo kimoja cha Habari jijini Dar es Salaam, leo, akisisitiza
kuwa, Jeshi la Polisi lipo imara kipindi hiki tunapoelekea katika uchaguzi wa
Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani, hivyo vyama vya
siasa vilivyotangaza kuanza kufanya mikutano ya hadhara kabla ya muda
Jeshi lake litavishughulikia ipasavyo.
“Hii naomba eleweka na pia iwekwe akilini, mikutano ya hadhara bado
haijaruhusiwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ni kosa kufanya
mikutano ya hadhara kabla ya tarehe ya kufanya mikutano ya hadhara
pamoja na kampeni haijatangazwa, jana kuna chama kimetangaza kuanza
kufanya mkutano wa hadhara, sasa waendelee na mipango yao, alafu
tuone nini kitawatokea,” alisema Lugola.
Waziri Lugola alisema Serikali haiwezi kuchezewa na kamwe wanaotaka
kuichezea watashughulikiwa pamoja na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu
wa sheria za nchi.
“Kama wanataka kutikisa kiberiti cha Rais Magufuli watakikuta kimejaa,
wasithubutu kuichezea Serikali ya awamu hii, tupo imara na pia tutahakikisha tunalinda amani ya nchi hii kwa nguvu zote, na amani hii tuliyonayo hatuwezi kuipoteza kamwe,” alisema Lugola na kuongeza kuwa; “Nimekabidhiwa lindo hili na Rais Magufuli ili niweze kulilinda ipasavyo, hivyo basi, wanasiasa wasibiri muda wa kuanza kampeni, na sio kukurupa kufanya mikutano ya hadhara bila ya kufuata taratibu, hilo halikubaliki hata
kidogo.”
Pia Waziri Lugola, alipoulizwa kuhusu vituo vya polisi kutotoa dhamana saa
24 kama alivyoelekeza kwa nchi nzima, alishangazwa kama kuna baadhi ya
vituo hivyo kuendelea kuvunja maagizo yake, hivyo amewataka wananchi
wampigie simu kwa mwananchi yeyote atakaye onewa na askari au mtu
yeyote aliyopo ndani ya Wizara na Taasisi zake anazoziongoza.
“Mwananchi yeyote atakayenyimwa dhamana, au atakaye onewa,
akikisheni mnanipigia simu, na pia kuna njia nyingi za kutupa hapa
Wizarani kupitia mitandao yetu ya kijamii, tovuti pamoja na makamanda
mbalimbali walipo katika mikoa yote nchini,” alisema Lugola.
Aidha, Waziri Lugola amepiga marufuku tabia ya Watanzania kuchukua
sheria mkononi katika matukio yoyote yanayotokea nchini, alisema
kumvamia mharifu na kumpiga ni kosa kisheria pamoja na matukio
mengineyo.