Home Mchanganyiko Tafiti saba za magonjwa ya moyo zilizofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya...

Tafiti saba za magonjwa ya moyo zilizofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuwasilishwa katika mkutano wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza unaotarajia kufanyika wiki ijayo nchini Zambia

0

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo akiwaeleza wafanyakazi wa Taasisi hiyo (hawapo
pichani) kuhusu tafiti saba za magonjwa ya moyo zilizofanywa na Taasisi
hiyo ambazo zitawasilishwa katika mkutano wa kimataifa wa magonjwa
yasiyo ya kuambukiza utakaofanyika wiki ijayo nchini Zambia.

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Happiness Swai
akiwaeleza wafanyakazi wa Taasisi hiyo (hawapo pichani) kuhusu utafiti wa
shinikizo la damu na tatizo la kisukari uliofanywa na Taasisi hiyo ambao ni
moja ya tafiti saba za magonjwa ya moyo ambazo zitawasilishwa katika
mkutano wa kimataifa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza utakaofanyika
wiki ijayo nchini Zambia.

Wataalamu wa Afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
ambao walifanya tafiti saba za magonjwa ya moyo ambazo zitawasilishwa
katika mkutano wa kimataifa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza
utakaofanyika wiki ijayo nchini Zambia wakiwa katika picha ya pamoja mara
baada ya kuzielezea tafiti hizo kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo leo jijini Dar
es Salaam.

Picha na JKCI

*****************

Na Ales Mbilinyi – JKCI

28/08/2019 Tafiti saba za magonjwa ya moyo zilizofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) zinatarajiwa kuwasilishwa  katika mkutano wa wanasayansi, madaktari bingwa na wahudumu wa afya wanaotoka katika nchi za ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika utakaofanyika wiki ijayo nchini Zambia.

Tafiti hizo ambazo zimefanyika mwaka jana na mwaka  huu ni kuhusu  mwenendo wa mapigo ya moyo kwa mgonjwa, wagonjwa wenye moyo ambao uwezo wake wa kufanya kazi umepungua  jinsi wanavyozingatia matibabu kama walivyoshauriwa na madaktari, shinikizo la damu na tatizo la kisukari.

Tafiti nyingine zitakazowasilishwa ni upungufu wa nguvu za kiume katika jamii, uelewa wa sababu hatarishi za magonjwa ya moyo katika jamii,  magonjwa matatu kwa pamoja yaani moyo na figo kushindwa kufanya kazi  na upungufu wa damu mwilini.

Akizungumza kuhusu tafiti hizo Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo alisema tafiti hizo zimefanyika katika  mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka miwili na na kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

“Tumekuwa tukifanya tafiti mbalimbali kuhusu magonjwa ya moyo ambazo zinatusaidia kufahamu wagonjwa wetu pamoja na wananchi wanaotuzunguka wanakabiliwa na matatizo gani katika afya za moyo na hii inatusaidia kuweza kuboresha huduma zetu”,.

Akizungumza kuhusu mkutano huo wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza   Dkt. Pedro alisema kwa upande wa magonjwa ya moyo utawasaidia  kubadilishana matokeo ya huduma za matibabu wanazozitoa hasa tafiti zinazofanywa katika nchi mbalimbali  ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa.

Kwa upande wake Afisa uuguzi wa JKCI Jalack Milinga ambaye alishiriki katika kufanya tafiti hizo alisema  kwake ni mara ya kwanza kuhudhuria mkutano huo ambao utamsaidia kuongeza ujuzi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa moyo lakini pia kubadilishana uzoefu na wauguzi wenzake watakaoshiriki katika  mkutano huo.

“Utafiti wangu uliangalia jinsi ya uzingatiaji wa unywaji wa dawa za moyo kwa wagonjwa ambao mioyo yao haifanyi kazi vizuri. Hivyo naamini ushiriki wangu katika mkutano huu utaniwezesha kupata mbinu mpya za kusimamia  jukumu  la kuwasaidia wagonjwa wetu kuzingatia matibabu ili kupata matokeo bora ya tiba”, alisema Jalack.

Naye daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Smita Bhalia alisema ushiriki wa wataalamu kutoka Tanzania  umelenga kutoa matokeo ya utafiti uliofanywa hapa nchini na kuonesha baadhi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza jinsi yanavyoweza kusababisha magonjwa ya moyo ama magonjwa ya moyo yanavyoweza kupelekea mtu kupata magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza.

Malengo ya mkutano huo ni kwa nchi  washiriki kutoka  ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika kuona  jinsi ya kushirikiana katika kufanya tafiti za ndani, kuwa na  njia bora na za kisasa za matibabu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza  na kuwa na  mbinu mpya za kuweza kuzia magonjwa hayo.

Mkutano huo ambao hufanyika kila mwaka unatarajia kufayika mjini Living stone nchini Zambia kuanzia tarehe tano  hadi saba mwezi ujao ambapo mwaka jana mkutano kama huo ulifanyika jijini  Nairobi nchini Kenya.