Home Mchanganyiko RC MAKONDA KUWASILISHA MUSWADA WA MAPENDEKEZO YA MABADILIKO YA SHERIA YA MIRATHI...

RC MAKONDA KUWASILISHA MUSWADA WA MAPENDEKEZO YA MABADILIKO YA SHERIA YA MIRATHI KWA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA

0

***********

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda anatarajia kuwasilisha Muswada wa mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Mirathi na Sheria ya Ndoa kwa Waziri wa Katiba na Sheria ili ziweze kufanyiwa marekebisho kutokana na Sheria hizo kupitwa na wakati na kuonekana kuwa kandamizi kwa wanawake pindi Mume anapofariki jambo linalopelekea Mateso na Manyanyaso kwa Wajane.

RC Makonda amesema miongoni mwa Sheria kandamizi zinazotakiwa kufanyiwa mabadiliko ni Sheria ya Kiserikali ya Mirathi ya Mwaka1865, Sheria ya Mirathi ya Kimila ya Mwaka1963 na Sheria ya Mirathi ya Kidini ya Mwaka1963 ambazo kimsingi zimeonekana kuwa na Mapungufu makubwa na zimepitwa na wakati.

Aidha RC Makonda amevitaja vipengele anavyopendekeza kufanyiwa maboresho ni pamoja na kumpa uhalali Mke wa marehemu kushiriki katika vikao vya mgawanyo wa mali, mjane kupewa haki ya kurithi na kusimamia mali za marehemu, Mjane kutoondolewa kwenye nyumba wala Mali kuhamishwa, Usawa wa watoto katika kumiliki mali za marehemu bila kujali jinsia pamoja haki ya mtoto wa nje ya Ndoa kurithi Mali.

Vifungu vingine ambavyo RC Makonda ameeleza kuwa ni kandambizi kwa Mjane ni pamoja na kile kinachoruhusu Mjane kurithiwa na kile kinachomnyima Mwanamke haki ya kurithi ardhi ya ukoo.

RC Makonda amesema chimbuko la hayo yote ni Kongamano la Wajane zaidi ya 5,181 alilohitisha mwezi April ambapo katika kongamano hilo alipokea Kero na Malalamiko mbalimbali kutoka kwa Wajane jambo lililopelekea kuunda kamati iliyoshirikisha Wadau na Wataalamu mbalimbali kutoka Serikalini na Asasi za Kiraia waliopitia malalamiko hayo na kutoka na mapendekezo hayo.