******************
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amemtaka Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA) kushirikiana na TAMISEMI pamoja na viongozi wa Mkoa wa Tanga kufanya uchunguzi wa wizi wa mitihani ambao umefanyika katika miaka ya nyuma wilayani Kilindi.
Naibu Waziri ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu wilayani humo ambapo amesema uchunguzi huo ufanywe ili kujiridhisha kwamba wizi huo wa mitihani hauendelei kwani haipendezi kuwa na vijana wasomi wazuri ambao wamefaulu kwa njia za udanganyifu.
Ole Nasha amesema yeye kama msimamizi wa sera na sheria, suala la uvunjifu wa sheria na wizi wa mitihani haliwezi kumfurahisha kwani jambo hilo ni kosa. Amesema inasikitisha kuona wizi huo umefanyika na viongozi wanafahamu lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahusika wa wizi huo wa mitihani.
Aidha, Naibu Waziri amesema wilaya hiyo haijakaa vizuri kitaaluma kwani katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne ya mwaka 2017 kuelekea 2018 ufaulu ulishuka kutoka asilimia 85 mpaka 55. Amesema anguko hilo ni kubwa ambalo kama ukiwa msimamizi wa elimu linashtua na hivyo kuhitaji kujua sababu ya anguko hilo ili kuweza kuchukua hatua za kusaidia kutoka katika hali hiyo.
“Kwa bahati mbaya sababu ambazo mmezitoa si nzuri, ukisikia kwamba sababu tumezuia walimu wasitoe majibu kwa wanafunzi hiyo sio sababu kwani hilo ni kosa katika sheria hii. Inamaanisha kwamba Kilindi mitihani imekuwa ikiibiwa, viongozi wanajua na hakuna hatua zinazochukuliwa,” amesema Ole Nasha.
Amesema usimamizi wa elimu katika wilaya ya Kilindi si mzuri na amemtaka Afisa Elimu wa Mkoa wa Tanga kuhakikisha anaangalia changamoto zilizopo katika wilaya hiyo na kuona namna ya kuweka mikakati ya kutatua changamoto hizo.
Aidha, Ole Nasha amesema Serikali imepeleka fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya ujenzi wa mindombinu katika wilaya hiyo na amesisitiza kuwepo na usimamizi mzuri wa fedha hizo na kusisitiza kwamba fedha hizo zinapelekwa katika wilaya kwa ajili ya kuboresha elimu hivyo haipendezi zisitumike kufanyia kazi iliyokusudiwa ama kuchelewesha kutekeleza miradi.
Naibu Waziri huyo ameonyesha wasiwasi wa kuchelewa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kuanzishwa kidato cha tano katika shule za Mafisa na Kikunde ambao fedha zake zilitumwa toka mwezi wa kwanza na kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Sauda Mtondoo kufuatilia sababu za ucheleweshaji wa mradi huo pamoja na kujihakikishia ukweli wa taarifa iliyotolewa kuhusu ujenzi huo ili kujiridhisha.
Naye Mtondoo akitoa taarifa ya Sekta ya Elimu katika wilaya hiyo iliyoonesha kushuka kwa kwa ufaulu katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne ya mwaka 2017 kuelekea 2018, amesema kushuka huko kulitokana na kuzibwa mianya ya udanganyifu na wizi wa mitihani uliokuwa ukiendelea katika wilaya hiyo kwa miaka mingi.
Mtondoo amesema sababu nyingine ni kuwepo kwa mgomo baridi uliokuwa ukifanywa na walimu wa wilaya hiyo kutokana na kutotekelezewa madai yao ikiwemo kutopandishwa madaraja jambo ambalo wilaya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi wamelitatua na walimu sasa wameacha mgomo huo.
Aidha, Mbunge wa Kilindi, Omari Kigua amekiri kuwepo kwa tabia ya walimu kuwapa wanafunzi majibu ya mitihani na kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye baada ya kufika Kilindi na kuona tatizo hizo la wizi wa mitihani aliweka mikakati ya kuhakikisha mianya hiyo inazibwa ili kuzuia wizi huo.
“Ni ukweli usiopingika kwamba wizi wa mitihani ulikuwepo, Kilindi tunataka kupata wasomi wazuri na si wasomi wa wizi wa mitihani, hatuwezi kuficha ukweli kwamba walimu walikuwa na tabia hiyo. Ni ngumu kuamini kwamba kuongeza usimamizi wa mitihani ndo sababu ya kufeli kwa wanafunzi,” amesisitiza Kigua.