NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MKUU wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama amesema, kuna kila sababu ya kuanzishwa kwa masomo ya ufundi stadi katika shule za sekondari ili kuendeleza vipaji vya wanafunzi ambao uwezo wao kitaaluma ni mdogo.
Ameshauri, wakati mwingine wanafunzi wanalaumiwa kufanya vibaya kwenye masomo yao lakini wana vipaji vya ufundi hivyo na wao wangepatiwa madarasa ya ufundi ingesaidia kuongeza ufaulu .
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa mafunzo ya siku moja kwa walimu wa shule za sekondari tano ambazo zimepata matokeo mabaya pamoja na tano za binafsi zilizofanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha nne katika, Halmashauri ya Mji wa Kibaha ili kubadilishana uzoefu na kutumia mbinu stahiki za kufaulu.
“Baadhi ya wanafunzi uwezo wao darasani siyo mzuri lakini wako vizuri kwenye masuala ya ufundi hivyo kuna haja ya kuwa na madarasa ya ufundi ili wasikose vyote”
“Ukiwalazimisha wasome masomo ya darasani hawataweza hivyo nafasi yao ni kuwapeleka madarasa ya ufundi,” alishauri Assumpter.
Optuna Kasanda kaimu ofisa elimu sekondari ,Halmashauri ya Mji Kibaha alisema kuwa matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2018 yanatoa uhalisia kuwa shule za sekondari binafsi zimeshika nafasi ya kwanza mpaka ya 13 huku zile za serikali zikiwa zimeshika nafasi ya 14 hadi 33 kati ya 33 zilizofanya mtihani wa taifa za Halmashauri ya Mji.
Alifafanua, licha ya matokeo hayo kuonyesha shule binafsi zimefanya vizuri lakini hata zile za serikali nazo zimeongeza ufaulu na hiyo inatokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na madarasa ,madawati na mbinu mbalimbali za ufundishaji.
Nae Mwalimu Zamda Komba moja ya waandaaji wa mafunzo hayo alisema lengo ni wao kufanya vizuri licha ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili walimu wa shule za sekondari za sekondari ambazo hata hivyo wanaendelea kukabiliana nazo.
Alitaka kuutambua mfumo wa elimu usio rasmi ili nao ujumuishwe kwenye mfumo wa elimu ukiwa ule wa vyuo vya ufundi stadi ili na wale wanaopitia kwenye mfumo huo wawe rasmi.
Awali mwalimu wa shule ya Sekondari Bundikani Abdala Likava alisema kuwa baadhi ya masomo yamekuwa yakiwafanya wanafunzi wasifanye vizuri na kupata matokeo mabaya.