Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Kelvini Mhina akitoa elimu juu ya Mahakama Inayotembea kwa wananchi waliofika Mahakamani hapo kupatiwa huduma mbalimbali. (Picha na Aziza Muhali)
Baadhi ya wananchi waliofika kupatiwa huduma za kimahakama katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakisikiliza maelezo juu ya utendaji kazi wa Mahakama Inayotembea.
Na Aziza Muhali
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es Salaam leo imetoa elimu juu ya Mahakama Inayotembea kwa wananchi ili waweze kuifahamau na kupata huduma zinazotolewa na Mahakama hiyo.
Akizungumza na wananchi ambao walifika katika Mahakama hiyo ili kupata huduma mbalimbali, wakati wa utoaji wa elimu kwa umma, Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Kelvin Mhina, amewataka wananchi kufikisha ujumbe wa Mahakama Inayotembea, kwa wananchi wengine ili waweze kufahamu jinsi Mahakama hiyo inavyofanya kazi.
“Mahakama hii ni Mahakama inayotembea na iliyokamilika inayowafikia wananchi katika makazi yao lengo likiwa ni kuboresha na kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi, “alisema Mhe.Mhina.
Aliongeza kuwa maeneo yatakayohudumiwa na mahakama hiyo ni wakazi wa Bunju A ambapo Mahakama hiyo itatoa huduma katika viwanja vya Ofisi ya Serikali za Mitaa, Kibamba, Viwanja vya Ofisi ya Wilaya ya Kinondoni, Chanika, pembeni ya Kituo kipya cha Polisi Chanika, Buza, eneo la kituo cha Mabasi Buza.
Kwa upande wake Karani Mkuu Kitengo cha Jinai, Imakulata Konala ambaye pia ni Msaidizi Mkuu wa Kumbukumbu kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, amewataka wananchi hao kuepuka kupewa huduma na watu wasiojulikana kisheria ,bali wawatumie watumishi wa Mahakama ambao huvaa vitambulisho vya kazi.