Baadhi ya wanachama wa UVCCM Mjini Babati Mkoani Manyara wakishiriki kuchangia damu kwenye ofisi ya CCM Tawi la Bagara.
***************
JAMII yatakiwa kuwa na mwamko wa kuchangia damu ili kuwasaidia wahitaji waliopo kwenye hospitali mbalimbali nchini, wakiwemo wanawake wenye ujauzito na majeruhi wanaopata ajali.
Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) mkoani Manyara, Moses Komba aliyasema hayo wakati akielezea mpango wao wa kuchangia damu ya kuwasaidia majeruhi wa ajali iliyotokea Morogoro.
Komba alisema umoja huo unawaomba wananchi kuwa na tabia ya kujitokeza kuchangia damu kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji mbalimbali.
Alisema viongozi, wanachama na vijana wa chama chao wanapaswa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya majeruhi waliopata ajali ya moto mkoani Morogoro.
“Tunapaswa kuchangia damu kwani huu ndiyo utamaduni wa Watanzania kushirikiana wakati wa shida na raha bila kujali dini, kabila, rangi, itikadi ili kuonyesha umoja wetu kwa kusaidia ndugu zetu,” alisema Komba.
Katibu wa UVCCM mkoani Manyara, Daniel Muhina alisema wamepata uniti 58 za chupa za damu na wanaendelea na uchangiaji damu hadi Agosti 31.
Muhina alisema shughuli za uchangiaji damu zinaendelea mkoa mzima ambapo mjini Babati ni kwenye ofisi za CCM Bagara na halmashauri ya wilaya ya Babati ni kituo cha afya Magugu.
Alisema sehemu nyingine ni ofisi ya CCM ya wilaya ya Hanang’, hospitali ya wilaya ya Mbulu, kituo cha afya Orkesumet wilayani Simanjiro na hospitali ya wilaya ya Kiteto.
Mmoja kati ya vijana hao, Carol Gisimoy alisema wanaungana na watanzania wengine nchini katika kuwasaidia kuchangia damu majeruhi wa ajali hiyo ya Morogoro.
Agosti 10 mwaka huu ajali ya lori la mafuta ilitokea Msamvu mkoani Morogoro ambapo watu 101 walifariki dunia na majeruhi 12 wamelazwa hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.