TIMU ya Lipuli FC ya Iringa imeanza vyema michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar jioni ya leo Uwanja wa Samora mjini Iringa.
Mabao ya Lipuli FC leo yamefungwa na Paul Materaz dakika ya tisa, Daruesh Salibiko dakika ya 10 wote wakimalizia pasi za Issa Ngoah na Seif Karihe dakika ya 68, wakati bao pekee la Mtibwa Sugar limefungwa na Ismail Mhesa dakika ya 78.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, bao pekee la Hassan Kapalata dakika ya 25 lilitosha kuipa ushindi wa 1-0 Mwadui FC dhidi ya Singida United Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Mechi za jana Kagera Sugar ya Bukoba ilishinda 2-0 dhidi ya wenyeji, Biashara United Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara, mabao ya Yussuf Mhilu dakika ya 14 na Awesu Awesu dakika ya 90 na ushei katika mchezo ambao wenyeji walikosa penalti iliyopigwa na Jarome Lambere.
Wageni Polisi Tanzania walishinda 1-0 dhidi ya Coastal Union bao pekee la Mohamed Mkopi dakika ya 33 Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wakati Mbeya City imetoa sare ya 0-0 na mahasimu wao wa Jiji, Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Nayo Mbao FC ililazimishwa sare ya 1-1 na wapinzani wao wa Jiji, Alliance FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. Mbao FC walitangulia kwa bao la Paschal Frank dakika ya 28, kabla ya Ibrahim Said kujifunga dakika ya 90 na ushei kuipa Alliance bao la kusawazisha.
Nayo Namungo FC ikaanza vyema kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mabao yake yote yakifungwa na Lucas Kikoti huku la wageni likifungwa na Omar Ramadhan. Ndanda walimaliza pungufu baada ya Hemed Koja kutolewa kwa kadi nyekundu.