Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara Simba wameshindwa kusonga mbele katika michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya kutoka sare ya kufungana 1-1 na U Desportiva Do Songo (UD SONGO) kutoka Msumbiji na kuwatupa nje .Mchezo uliomalizika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wageni walianza kwa kasi dakika za mwanzo kwa kuwasambuliaji wenyeji huku wakikosa mabao mawili ya wazi hata hivyo Simba waliamka na kushambaulia kwa nguvu.
Mnamo dakika ya 13 Nahodha wa UD SONGO aliwanyanyua wageni akifunga bao kwa mpira wa faulo ulioenda moja kwa moja na kumshinda Aisha Manula aliyeshindwa kupaanga vizuri safu yake ya ukuta.
Baada ya kufungwa bao hilo Simba walianza kulishambulia lango la UD SONGO kama nyuki hata hivyo kipindi cha kwanza hawakuweza kupata bao.
Kipindi cha pili timu zote zilianza kwa kushambuliana kwa zamu huku zikifanya mabadiliko hata hivyo wageni waliweza kunufaika zaidi.
Beki kisiki wa timu ya Taifa Stars Erasto Nyoni,aliisawazishia Simba kwa njia ya mkwaju wa Penalti dakika ya 85 hata hivyo bao hilo halikuweza kuwa na faida kwa wenyeji.
Hadi dakika 90 za Mwamuzi kutoka nchini Rwanda Jean Claude Ishimwe,anapuliza kipenga cha mwisho UD SONGO wamesonga hatua ya 32 na kuwatupa nje Simba ambao msimu uliopita waliweza kuishia hatua ya Robo Fainali kwa kufungwa na TP Mazembe mabao 4-1.
Tegemeo kwa Tanzania kwa sasa limebaki kwa timu tatu ambazo zimesonga mbele Yanga bado wapo katika klabu Bingwa huku kwenye shirikisho Azam FC na Malindi FC kutoka visiwani Zanzibar