Na Mathew Kwembe, Arusha
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameyafunga Mashindano ya 19 ya michezo ya shule za Sekondari kwa nchi za Afrika Mashariki (FEASSSA) kwa kuahidi kuwa mwakani timu kutoka Tanzania zitaleta upinzani mkali kulinganisha na mwaka huu.
Akizungumza kwenye sherehe za kuhitimisha mashindano hayo zilizofanyika leo leo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Mhe.Mwakyembe amewatahadharisha wenyeji wa mashindano hayo mwakani nchi ya Kenya kuwa wakae tayari kwani timu kutoka Tanzania zitakuja kwenye michuano hiyo kwa kishindo.
Amesema kuwa katika mashindano ya FEASSSA mwakani ambayo yamepangwa kufanyika katika mji wa Kakamega nchini Kenya, timu za kutoka Tanzania zitaleta upinzania mkali kwani zitakuja kwenye mashindano hayo zikiwa zimejiandaa vizuri.
“Napenda kukuhakikisha Rais wa FEASSSA kuwa tutaziandaa timu zetu vizuri ili mwakani ziweze kushinda makombe mengi,” amesema Mhe.Mwakyembe.
Aidha Mhe.Mwakyembe amezitaka timu za nchi wanachama zilizoshiriki mashindano haya kuhakikisha kuwa zinafanya maandalizi ya kutosha kwani bila hivyo zitaendelea kutofanya vizuri.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bi Odilia Mushi amesema jumla ya washiriki 3600 wameshiriki mashindano ya FEASSSA, wakiwemo washiriki kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Uganda, Zanzibar,Tanzania na nchi ya Malawi walishiriki michuano hiyo kama mgeni mwalikwa.
Amesema michuano ya mwaka huu mbali na kuwashirikisha wanafunzi wa sekondari pia iliwahusisha wanafunzi wa shule za msingi, wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Bi Mushi ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha kuwa kuwa kila mwaka wawashirikishe wanafunzi walio kwenye mahitaji maalum.
“Natoa wito ushirikiano huu ambao tumeuonyesha Afrika Mashariki kwa kuuonyesha kwa wenzetu hawa wenye mahitaji maalum,” amesema.
Ameongeza kuwa michezo hii imefanyika kwa ufanisi mkubwa ambapo kila nchi ilipata fursa ya kuonyesha vipaji vyao, na kuongeza kuwa changamoto zilizojitokeza mwaka huu zitakuwa kichocheo kwa ajili ya kufanya vizuri katika mashindano ya mwakani.
Naye Rais wa FEASSSA bwana Justus Mugisha amesema kuwa kuanzia mwakani jina la mashindano hayo litabadilika kutoka kuwa FEASSSA hadi FISSA na kuongeza kuwa timu zitakazoshiriki mashindano hayo zimeongezewa siku moja zaidi ili kutoa fursa kwa wawakilishi wa kila nchi kwenda kwenye utalii wa ndani.
Aidha bwana Mugisha amezitaka nchi wanachama kuhakikisha kuwa zinafanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kushiriki mashindano mengine ya FEASSSA kwani bila kufanya hivyo itakuwa ni ndoto kwa timu hizo kushinda michuano hiyo.
Akizungumzia michuano hiyo, bwana Mugisha amesema kuwa mashindano ya mwaka huu yalikuwa ni magumu kulinganisha na mashindano yaliyopita na hivyo akataka timu ambazo hazikufanya vizuri mwaka huu ziende zikajiandae kwa ajili ya michuano mingine kama hiyo itakayo fanyika mwakani nchini Kenya.
Kabla ya kufunga mashindano hayo Waziri Mwakyembe alipata fursa ya kushuhudia pambano kali la fainali la mpira wa miguu baina ya timu mbili za Uganda.