Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) Selemani Jafo, ametangaza rasmi siku ya uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa kuwa utakuwa siku ya tarehe 24 Novemba, 2019, uchaguzi utakao fanyika kote hapa nchini.
Waziri Jafo ametangaza siku hiyo Jijini Dodoma, wakati wa mkutano na wakuu wa mikoa wakati wa kuwapa maelekezo na makabidhiano ya nyaraka zinazohusiana na uchaguzi huo amesema ametangaza uchaguzi huo kwa mujibu wa sheria.
Amesema uchaguzi utafanyika novemba 24, 2019 kuanzia majira ya saa mbili kamili(12:00)hadi saa kumi kamili (10:00) jioni na tayari maandalizi yote tayari yamekamilika kwa ajiri ya uchaguzi huo.
“Tangu kurejeshwa kwa mamlaka za Serikali za Mitaa katika mfumo wa utawala kupitia sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 na sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288, uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya Mtaa, Kijiji na Kitongoji”
“Umekuwa ukifanyika katika kila kipindi cha miaka mitano, uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwezi Oktoba mwaka 2014 na hivyo uchaguzi mwingine unatakiwa kufanyika mwaka 2019, na tarehe hiyo ni Novemba 24, mwaka huu” amesema Jafo.
Amesema uchaguzi huu unaongozwa kwa kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa katika mamlaka za Wilaya na mamlaka za Miji, kwa mujibu wa matangazo ya Serikali Na. 371, 372 373 na 374 ya mwaka 2019.
Amebainisha nafasi zitakazo gombewa katika uchaguzi huo, “Mwenyeviti wa Kitongoji katika mamlaka za Miji Midogo, kwa nafasi hiyo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za Miji Midogo za mwaka 2019 (Tangazo la Serikali Na. 371 la Mwaka 2019)”. Amesema.
Pia wengine ni wenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake) na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi la Wanawake) katika Mamlaka za Miji, kwa nafasi hizo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa kamati ya Mtaa katika Mamlaka za Miji za mwaka 2019 (Tangazo la Serikali Na. 372 la Mwaka 2019).
Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa halmashauri ya Kijiji (Kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake), Wajumbe wa halmashauri ya Kijiji (kundi la wanawake) na Wenyeviti wa Vitongoji katika mamlaka za Wilaya.
Kwa nafasi hizo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya za Mwaka 2019 (Tangazo la Serikali Na. 373 la Mwaka 2019); na
Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wahalmashauri ya Kijiji (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake), Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake) na Wenyeviti wa Vitongoji katika Mamlaka za Miji.
Kwa nafasi hizo, Uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji za Mwaka 2019 (Tangazo la Serikali Na. 374 la Mwaka 2019).
Waziri Jafo amewataka Wakuu wa mikoa kuhakikisha wanasimamia na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya uchaguzi huo sambamba na kuhakikisha vifaa vinafika kwa wakati maeneo husika na kuratibu uchaguzi huo, na amebainisha kampeni zitaanza siku saba kabla ya uchaguzi huo.
Akiongea kwa niaba ya wakuu wa mikoa, Mkuu wa Mkoa wa Singida Rehema Nchimbi amesema kama wakuu wa mikoa wamepokea maelekezo yote na wataenda kuyafanyia kazi pamoja na kuhakikisha uchaguzi huo unaenda kama ulivyopangwa na kuhakikisha vifaa vinafika kwa wakati.