Jengo la vyumba viwili vya madarasa linaloendelea kujengwa katika shule ya msingi Nsemulwa.
Wanafunzi wa darasa la chekechea wakiwa katika foleni ya uswahishwaji wa kazi zao.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la tatu wakionekana kwa nje ya darasa baada ya kukosa nafasi ndani ya darasa.
****************
Na Mwandishi wetu, Katavi
Msongamano mkubwa wa wanafunzi katika madarasa katika shule ya msingi Nsemulwa yenye wanafunzi 3,603 iliyopo katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi; unapelekea baadhi ya wanafunzi kujifunza wakiwa nje ya darasa kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa na hivyo kupelekea mwamko duni wa wanafunzi kwenda shule.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Emmanuel Mbogo alisema shule hiyo yenye vyumba 11 tu vya madarasa ina wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba wanaoingia kwa awamu mbili.
Mwalimu Mbogo aliongeza kuwa madarasa yaliyo na msongamano mkubwa zaidi ni kuanzia darasa la chekechea hadi darasa la nne, ambapo walimu wamekuwa wakifundisha katika mazingira magumu kutokana na msongamano wa wanafunzi
Aidha kuhusu wanafunzi wanaosoma wakiwa nje ya darasa wakati wenzao wako ndani amesema wanafunzi wanaochelewa kuingia darasani ndio wanakosa nafasi na kuongeza kuwa hali inachangia katika utoro kwani wanafunzi wanakata tama kusoma katika hali hiyo
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo waliopata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari wametoa wito kwa wadau kujitolea kuwatatulia changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Afisa Elimu msingi wa Manispaa ya Mpanda bwana Godfrey Kalulu amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo amesema wadau mbalimbali wamejitokeza kujenga vyumba vya madarasa.
Aidha amesema Manispaa imepokea shilingi milioni 129 kutoka serikali kuu kwa ajili ya kumalizia majengo yaliyojengwa na wananchi katika shule mbalimbali katika manispaa hiyo.
Bwana Kalulu amesema shule ya Msingi Nsemulwa imepokea kiasi cha shilingi milioni kumi kwa ajili ya kumalizia jengo la vyumba viwili vya madarasa na jengo la utawala ambalo liko katika hatua ya umaliziaji.