Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bi. Vickness Mayao akizungumza na vyombo vya habari leo Jijini Dodoma kwa ajili ya kutoa mwelekeo wa zoezi la uhuishaji Mashirika amabayo awali yalijisajili chini ya Sheria nyingine.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
…………….
Na Mwandishi Wetu Dodoma.
Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii imetoa muda zaidi wa zoezi la usajili na uhuhishaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo awali yalijisajili kwa Sheria ya Makampuni, Bodi ya Wadhamini na sheria ya Jumuiya za Kiraia chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambazo kwa sababu tofouti hazijakamilisha zoezi la uhuishaji kwa mujibu wa Sheria no. 3 ya mwaka 2019.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dodoma Msajili wa NGOs Nchini Bi. Vickness Mayao amesema kimsingi kazi hii inahusu yale mashirika ambayo hayajakamilisha zoezi la kuhuisha vyeti vyao kwa mujibu wa Sheria na Wizara imeona ni vyema kuendelea na zoezi hilo baada ya kuwa imefanya hivyo katika Kanda tano hapa nchini.
“Tunaendelea na zoezi la usajili huu ambao kisheria unakamilika tarehe 30 Augusti 2019 kama Sheria no.3 ya mwaka 2019 inavyoelekeza ili kutoa nafasi zaidi kwa Mashirika yaliyosalia ambayo kwa namna moja au nyingine bado hayajakamilisha usajili wake na ifikapo mwisho wa mwezi huu kila Shirika litabaki katika Sheria yake”. Aliongeza Bi. Mayao.
Aidha Bi. Mayao amesema kuwa Ofisi ya Msajili wa NGOs tayari imetoa orodha ya awali ya Mashirika ambayo yameondolewa kwenye Daftari la Msajili wa Mashirika Yasiyo kuwa ya Kiserikali ambayo pia yanatakiwa kuhamia katika Sheria nyingine akiongeza kuwa orodha hiyo tayari imewekwa kwenye tovuti ya Msajili wa NGOs.
Bi. Mayao ametaja idadi ya Mashirika hayo kuwa ni 158 na inatarajia kuongezeka kadili zoezi la kuyatambua Mashirika hayo linavyoendelea na kusisitiza kuwa orodha iliyopo ni ya wali na kuyataka Mashirika hayo kufanya haraka kuhuisha usajili wao kama Sheria mpya inavyosema kwani kushindwa kufanya hivyo maana yake shirika husika litakuwa limefutwa.
Msajili wa NGOs ameongeza kuwa zoezi la uhuishaji limefanikiwa kwa asilimia 85 baada ya kuwa limefanyika katika kanda tano ikiwemo Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati , Kanda ya Kaskazini, Pwani na Nyanda za Juu Kusini na sasa zoezi hili linaendelea mjini Dodoma kwa ajili ya Mashirika ambayo bado yamesalia na zoezi hili linaendelea kwa kushirikiana na wale wanaosimamia Sheria nyingine.
Zoezi la uhuishaji Mashirika linafanyika kwa miezi miwili kwa mujibu wa Sheria no.3 ya mwaka 2019 na tayari limekamilika katika Kanda tano lakini linaendelea kukamilika Jjini Dodoma ili kutoa fursa ya ziada kwa Mashirika ambayo bado hajakamilisha zoezi la uhuishaji usajili kwake kabla ya kuondolewa usajili kama takwa la kisheria lilivyo katika Sheria hiyo.