Waziri wa Madini Dotto Biteko akizungumza na wadau wa madini, wapili kulia ni Rais wa FEMATA, John Bina
Ofisa habari na mawasiliano wa shirikisho la vyama vya wachimbaji madini nchini FEMATA, Dk Bernard Joseph akizungumza na wadau wa madini ya dhahabu eneo la Bassotu Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara.
Waziri wa Madini Dotto Biteko (katikati) akiwa na Rais wa FEMATA, John Bina (kushoto) na Kamishna wa Tume ya madini wa FEMATA, Haroun Kinega.
……………………..
SHIRIKISHO la vyama vya wachimbaji madini nchini (FEMATA) wakiongozwa na Rais wao John Bina wanatarajia kufanya mkutano mkuu wa sita jijini Tanga.
Kwa mujibu wa afisa habari na mawasiliano wa FEMATA, Dkt Bernard Joseph mkutano huo mkuu wa sita unatarajia kufanyika Agosti 31 mwaka huu kwenye hotel ya kitalii ya Tanga Beach Resort jijini Tanga.
Dkt Joseph alisema mgeni rasmi siku ya ufunguzi wa mkutano huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Madini, Dotto Mashaka Biteko.
Alisema mambo mbalimbali yenye manufaa ya wadau wa madini yatajadiliwa na kupitishwa kwenye mkutano huo ambapo washiriki wanapaswa kuwasiliana na wenyeviti wa vyama vya wachimbaji madini wa mikoa au Mtendaji Mkuu wa FEMATA.
Alisema FEMATA ni shirikisho la vyama vya wachimbaji madini nchini linalowaunganisha wachimbaji madini, wafanyabiashara na wadau wa madini na Serikali.
“FEMATA huendesha mafunzo ya elimu na ujuzi wa madini, biashara ya madini, changamoto na athari za mazingira kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Madini,” alisema Dkt Joseph.
Alisema FEMATA imeundwa na vyama vya mikoa vya madini na Wadau mbalimbali vikiwemo vyama vya wafanyabiashara na wadau wa Madini.
Alisema FEMATA ni uwakilishi katika vyama vya mikoa vya madini (REMAs) kwenye masuala mbalimbali ya madini.
Alisema FEMATA ni chombo cha utetezi wa wachimbaji madini katika kuongeza ufanisi na masilahi ya wachimbaji na haki zao.
Alisema FEMATA ni
shirikisho linalowakilisha vyama vya kimkoa vya wachimba madini (REMAs) katika kuwaunganisha wachimbaji madini na wadau wa uchimbaji madini na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa kimaendeleo.
Alisema dira na malengo ya FEMATA ni kutengeneza mazingira rafiki kwa wachimbaji madini, wadau na serikali ili kuleta ufanisi katika sekta ya madini na ukuzaji wa pato la taifa.
“Sisi FEMATA dira yetu ni kuhakikisha nchi na wachimbaji madini wananufaika na madini yaliyopo,” alisema Dkt Joseph.
Dkt Joseph alisema
wanachama wao ni wachimbaji au wamiliki wa migodi kutoka katika mikoa yote nchini, wafanyabiashara na wadau mbalimbali na wanaotaka kujiunga wanapaswa kuwasiliana kupitia [email protected]
Alisema faida za kujiunga na FEMATA,
zipo nyingi ikiwemo kupata mafunzo mbalimbali yanayohusu madini, biashara ya madini, utatuzi wa changamoto mbalimbali, uwakilishi na utetezi kwa wanachama katika maeneo ya madini.
Alisema FEMATA ni kiungo muhimu katika kuwaunganisha wachimbaji madini na serikali ili kuhakikisha shughuli zao zinakwenda vizuri kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
“FEMATA Ni Shirikisho linalowakilisha vyama vya kimkoa vya wachimba madini katika kuwaunganisha na serikali,” alisema Dkt Joseph.