Matundu hayo manane ya vyoo vilivyogharimu sh. 20,304,800, vimejengwa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TD&CF) Tawi la Tanzania kwa ufadhili wa Charty Walfare Aid ya Australia.
Akikabidhi vyoo hivyo kwa uongozi wa hospitali hiyo jana Mwenyekiti wa TD &CF, Alhaji Sibtain Meghjee alisema taasisi hiyo inafanya shughuli za kijamii kwenye sekta za maji, elimu na afya iliguswa na changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo inayoikabili hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Mwanza.
Alisema hospitali ya Sekou Toure iliyojengwa miaka ya 70 ikiwa kituo cha afya ilikuwa na matundu manne tu ambayo hayakidhi mahitaji na kwa kutambua umuhimu wa afya bora kwa jamii inayohudumiwa hapo iliamua kujenga matundu manane kati ya 20, ambapo matundu 12 yajengwa baadaye ili kumudu kuhudumia watu zaidi ya 500 kwa siku.
Meghjee alisema dhamira ya taasisi hiyo ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha afya za wananchi na kuwaepusha na maradhi ya kuambukiza na kuwafanya kuwa na afya bora kuelekea uchumi wa kati wa viwanda, sababu bila afya njema ni vigumu kufikia ndoto hiyo.
“Nina furaha kuwafahamisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa matundu 8 ya vyoo umekamilika na niko tayari kuvikabidhi vianze kutumika vikiwa na vifaa vya usafi, tenki la maji la ujazo wa lita 5000.Awamu ya pili ya ujenzi utaanza wiki sita baadaye ukihusisha matundu 12 ili kukamilisha 20 yakiwemo ya watu wenye ulemavu, watumishi na wazee wa jinsia zote,”alisema.
Mwenyekiti huyo wa TD & CF alisema ili vyoo hivyo vidumu aliuataka uongozi wa hospitali hiyo kusimamia kwa dhati ili mundombinu yake isiharibiwe kwa sababu yampo maeneo mengi waliyosaidia kujenga vyoo miundombinu yake imehabiriwa.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo wa vyoo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure Dk. Bahati Msaki, alisema inahudumia watu 500 hadi 700 kwa siku hivyo msaada huo umekuja muda muafaka kwa sababu namba ya wahitaji ni kubwa.
“Kwa niaba ya Bodi na uongozi wa hospitali tunashukuru sana The Desk & Chair kwa msada huu wa vyoo matundu 8 ambayo yamegharibu fedha nyingi.Bado taasisi hii inaendelea kujenga mengine 12 ili kukamilisha matundu 20, ili kukidhi mahitaji makubwa ya wagonjwa na wasindikizaji pamoja na watumishi”alisema Dk. Bahati.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo imefanya mambo mengi kwenye hospitali hiyo kwa kujenga jengo la kupumzikia wananchi wanaokuja kuona waagonjwa pamoja na vyoo matundu saba, lakini pia imejenga vyoo matundu manne kwenye jengo la kuhifadhia maiti.
Hata hivyo, mbali na changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo kwa wagonjwa wan je, pia wodi nyingi zina changamoto hiyo na kuomba watu wengine wenye kuguswa na hali hiyo kuiga mfano wa The Desk & Chair ili kusaidia kujenga miundombinu ya vyoo hospitalini hapo.