****************
Na Abraham Nyantori-MAELEZO
Wakati vikao tangulizi vya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) vinafikia ukingoni mwishoni mwa wiki na kutoa nafasi kwa Marais wa SADC kukutana katika Mkutano wao wa kilele Agost 17 na 18, wafanyabiashara wa Tanzania na ujumbe wa wafanyabiashara wa Afrika Kusini wamekutana wakiongozwa na Marais wao Cyril Ramaphosa na Dkt. John Magufuli.
Mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar Es Salaam mbali na kuwakutanisha sekta binafsi, umewaleta pamoja Mawaziri wa sekta mbalimbali nchini, taasisi za umma na binafsi za Tanzania na Afrika Kusini, ukiwa ni jukwaa la pili kwa nchi hizo kuongea kuhusu fursa za biashara, uwekezaji na ukuzaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda Huku kila upande ukionyesha ari ya kuongeza ushirikiano kwa mataifa haya.
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli ameeleza mahusiano ya kibiashara baina ya Tanzania na Afrika Kusini, ambapo yanaonekana kukuwa kwa kasi, huku akitolea mfano miradi ya huduma na uuzaji wa bidhaa kwenda Afrika Kusini ulikuwa toka dola za kimarekani 108.2 milioni mwaka 2017 hadi dola 437.2 milioni kwa sasa.
Rais Magufuli amesema wawekezaji toka Afrika Kusini wamefikia 228 na kuwekeza kiasi cha dola za kimarekani 806.5 millioni na kushika nafasi ya 13 kwa ukubwa wa uwekezaji, ambapo Tanzania katika nchi za SADC, mahusiano yake kibiashara yako juu na Afrika Kusini ukilinganisha na nchi wanachama.
Pamoja na Tanzania kujiimarisha katika kuboresha mihimili ya kujenga uchumi kama uboreshaji wa usafiri na usafirishaji; bandari, viwanja vya ndege, barabara na vivutio vya utalii, Dkt Magufuli amesema serikali yake inatambua sekta binafsi katika uwekezaji na hivyo imeboresha sheria mbalimbali na Mamlaka zinazohudumia wawekezaji na wafanyabiashara ili kufanikisha.
Wakati Tanzania inahimiza uwekezaji wa ujenzi wa viwanda nchini kwa wawekezaji wa nje na ndani, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa anatambua hatua ambayo nchi yake imefikiwa kiuchumi, lakini anaona ipo haja kwa bara la Afrika kuona jinsi ya kujenga nafasi za kazi na kujenga uchumi wa mataifa hayo kwa maisha ya watu wake.
Rais Ramaphosa anasisitiza watu wa Tanzania na Afrika Kusini kuendeleza mahusiano yao ya kihistoria kwa nchi zao katika kustawisha uchumi,huku jicho la pili likiangalia dunia kama sehemu ya kutegemeana.
Pamoja na kuwepo uhusiano wa kihistoria uliotokana najitihada za Tanzania kushirikiana na nchi za Kusini mwa Afrika katika harakati za ukombozi wa Afrika, mahusiano yamekuwa yakipanda kutoka mahusiano ya kisiasa na kuona fursa za uwekezaji katika miradi mbalimbali na biashara baina ya mataifa haya mawili.