Na.Alex Sonna,Mpwapwa
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2019 Mzee Mkongea Ally amegoma kuzindua mradi wa maji wa Mzase uliopo wilayani Mpwapwa kutokana na kasoro mbalimbali za mradi huo, ikiwamo kukosekana kwa vielelezo vya majibu ya vipimo vya mabomba kutoka maabara ya serikali.
Akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu ya mradi huo Mkongea amesema baada ya ukaguzi wao wameona kuna baadhi ya vitu walivyoomba kwenye mradi huo havipo lakini fedha zinaonyeshwa zilitengwa.
“ Tulifanya ukaguzi kwa pamoja tumeona kuna baadhi ya vitu vielelezo vyake havipo kama test za nondo kutoka maabara ya serikali haipo,test za zege haipo,test za bomba kutoka maabara ya serikali hazipo,ubaya wa hapa ni kwamba kazi hazikufanyika lakini kwenye certificate fedha zimelipwa,”amesema Mkongea.
Amesema kutokana na kasoro hizo inaonyesha utaratibu ulikiukwa kwa kufanya malipo hewa hivyo Mwenge wa Uhuru 2019 hauwezi kuzindua mradi huo.
Kutokana na kasoro hizo amemtaka mkuu wa Wilaya hiyo Jabir Shekimweri kumpa taarifa za mradi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa(TAKUKURU)wilaya ili ajiridhishe na matumizi ya pesa zilizotumika.
“Tunajua mkuu wa wilaya hili sio kosa lako wala sio kosa la waheshimiwa wabunge,kuna wataalam ambao wanataalum ya injinia kuweza kusimamia miradi hii ndio wanakiuka utaratibu,mh mkuu wa wilaya tunakukabidhi taarifa ya mradi ili umkabidhi afisa Takukuru,kila eneo liangaliwe ili kujiridhisha matumizi ya fedha na baada ya wiki mbili taarifa itumwe makao makuu ya Takukuru,”amesema.
Pamoja na kasoro hizo Mkongea amesema wameangalia ubora wa maji kwa mujibu wa vipimo vya maabara na vimeonyesha kwamba maji ni salama kwa matumizi hivyo wananchi waendelee kuyatumia.
Kwa upande wake waziri wanchi ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira George Simbachawene amesema kitendo hicho kimekuwa ni fundisho kwa wao wanaoongoza jamii na kwa wataalam ili wanapoyasikia mapungufu hayo waweze kusema na katika vikao vya halmashauri.
Simbachawene ambaye ni mbunge wa Kibakwe ametumia nafasi hiyo kusisitiza wananchi kutunza vyanzo vya maji kwa kuheshimu sheria iliyopo ya kutofanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji.
Akizungumza baada ya maelekezo hayo Shekimweri amesema wamepokea taarifa ya ukaguzi na watazingatia maelekezo yaliyotolewa na kuyafanyia kazi.
Mradi huo umegharimu kiasi cha sh mil 432.2 ukihusisha baadhi ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa kisima,nyumba ya mashine,ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji,ujenzi wa mlango,ofisi ya jumuiya ya watumiaji maji na njia ya umeme mpaka eneo la kisima.