Askofu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Kanda ya Mashariki Kati mwa Tanzania
(E.C.T) Mchungaji Joseph Phidelis Mngwabi akitoa neno kwa wahitimu wa kozi fupi ya
muziki kutoka Kanisa la Waadventista wa Sabato iliyofanyika katika Chuo cha Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).
Wahitimu pamoja na wageni mbalimbali wakimsikiliza Askofu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Kanda ya Mashariki ya Kati mwa Tanzania (E.C.T) Mchungaji Joseph Phidelis Mngwabi (hayupo pichani) wakati wa hafla ya wahitimu wa kozi fupi ya muziki kwa waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato.
Wahitimu wa mwaka wa tatu walikabidhiwa vyeti viwili, kimoja cha TaSUBa na kingine cha Kanisa lakini mwaka wa kwanza na wa pili walikabidhiwa cheti kimoja cha kitaaluma ambacho ni cha TaSUBa.
Kwaya ya wahitimu wa kozi fupi ya muziki ikitoa burudani kwa wageni mbalimbali
waliohudhuria mahafali hayo.
***********
Kanisa la Sabato limetoa pongezi kwa Umoja wa kanisa hilo kuanzisha mfumo wa
waumini wa makanisa kujifunza muziki katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni
Bagamoyo (TaSUBa) na kutoa wito wa kujitokeza kwa waumini kupata elimu ya muziki kwa ajili ya kumuimbia na kumtukuza Mungu.
Akizungumza katika mahafali hayo na kukabidhi vyeti kwa wahitimu wa kozi fupi ya muziki, Mwenyekiti wa Konferensi ya Kusini mwa Tanzania (SEC), Mchungaji Steven Ngusa, ambae alimwakilisha Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania (Southern Tanzania Union) Askofu Marwa Marekana, alisema wengi wanaliangalia suala hilo katika kwaya za Makanisa badala ya kwenda mbali zaidi katika muziki kwani nyakati zilizopita waimbaji wa nyimbo za kumtukuza Mungu walikuwa wakiimba bila kutambua taratibu kutoka kwa wataalam.
Mchungaji Ngusa aliwashukuru TaSUBa kwa kukubali kutoa mafunzo kwa waumini wa Kanisa bila kujali wakati wa likizo.
Alisema mafunzo hayo yalishirikisha majimbo karibu yote ya Kanisa la Sabato na
madhehebu mengine ya kanisa na kueleza kwamba wahitimu hao wamepata elimu hiyo na wasidhani kama wameshajua bali wameanza kujua na kuwataka kuendeleza zaidi muziki huo kwa kumuimbia Mungu.
“Mafunzo yaliyopatikana yawe chachu na ya matengenezo kwa waumini wengine
ambao hawana elimu ya muziki, pia napendekeza tuanzishe mfumo kwa kutoa waumini wawili kila sehemu ili tutekeleze matakwa,” alisema Mchungaji Ngusa.
Naye Mkufunzi wa muziki TaSUBa, Heri Kaare alisema Taasisi (TaSUBa) na Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania wameingia ubia ili kufundisha muziki (taaluma) kwa washiriki wa Kanisa hilo. hiyo imeingia ubia na Jimbo Kuu la Kusini Tanzania katika mahafali ya kwanza kwa wahitimu wa mwaka wa kwanza, wa pili na watatu.
Kaare alisema baada ya mafunzo hayo, wapo ambao walikuwa hawajui na wengine walikuwa na uelewa hafifu lakini baada ya kukamilisha mafunzo hayo sasa wana utaalamu wa muziki wa kuimba na kwa kutumia vifaa.
Mahafali haya ni ya kwanza ambapo jumla ya wahitimu walikua 15 baada ya
kuhudhuria mafunzo kwa miezi mitatu. Wahitimu hawa walipewa vyeti viwili, ambavyo ni cheti cha TaSUBa na cheti cha Kanisa. Aidha wahitimu wengine waliohitimu kwa mara ya pili na ya kwanza walikua 12.