*************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameagiza watendaji wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu katika vyama vya ushirika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi wote wa ushirika nchini wahakikishe wanaongoza vyama vya ushirika kwa kufuata Sheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013, kanuni na taratibu zilizopo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Agosti 8, 2019) katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima nane nane Kitaifa kwenye viwanja vya maonesho Nyakabindi mkoani Simiyu kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa Wanaushirika wote nchini kuhakikisha wanachagua viongozi wenye weledi, wachapakazi, waadilifu na wanao upenda ushirika ili ushirika uimarike na kuwa endelevu.
Amesema historia inaonesha kwamba miaka ya nyuma ushirika ulifanya kazi nzuri katika kusimamia uzalishaji, tija, uchakataji na masoko ya mazao. “Hata hivyo, ushirika ulianza kulegalega katika miaka ya 1980”.
Waziri Mkuu amesema kutokana na hali hiyo, Serikali iliamua kuanzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika kama chombo cha kusimamia shughuli za maendeleo ya ushirika nchini.
Amesema katika kuimarisha vyama vya ushirika nchini, tume hiyo imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa Vyama vya Ushirika ili kuzalisha kwa tija na kuongeza uzalishaji kutokana na matumizi ya zana bora za kilimo. Amesema vyama vya ushirika 33 vimekopeshwa trekta moja kwa kila chama kupitia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tume na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Bodi ya Pamba (TCB).
Pia, Waziri Mkuu amesema katika kuendeleza azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda, Vyama vya Ushirika vimeendelea kuwekeza katika miradi mingine ya kimaendeleo ambayo inaisaidia katika kuleta maendeleo.
“Hadi kufikia Juni 30, 2019 jumla ya Vyama vya Ushirika 104 vinamiliki viwanda vidogo kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao wanayoyazalisha hali ambayo imeleta tija kwa jamii inayozunguka maeneo hayo”.
Amesema hadi Desemba 2018, mikopo yenye thamani ya sh. trilioni 1.3 imetolewa kwa wanachama ikilinganishwa na sh. bilioni 902 iliyotolewa kufikia Desemba 2017. Akiba na amana za wanachama katika SACCOS zimefikia sh. bilioni 575 na hisa sh. bilioni 79.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu kwa mara nyingine, ametumia fursa hiyo kuwaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wafanye tena mapitio ya idadi ya Maafisa Kilimo waliopo Wilayani na kuwahamishia katika kata na vijiji ili kuimarisha usimamizi wa mazao.
Hivyo, Waziri Mkuu amesema ngazi ya Makao Makuu ya Wilaya wabaki wataalamu wawili akiwemo Mkuu wa Idara na msaidizi wake kwa ajili ya uratibu. Maafisa Kilimo wa Wilaya wawe na ratiba za kwenda vijijini kuwatembelea maafisa ugani ili kutatua changamoto zinazowakabili katika uendelezaji wa kilimo na hawapaswi kukaa maofisini.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Nane Nane ya mwaka huu inasema: – “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Nchi”. Kaulimbiu hiyo inakwenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukuza uchumi wa viwanda na biashara, ikilenga kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa na wakati huo huo kupunguza umaskini.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea na kukagua mabanda mbalimbali katika maoneosho hayo. Miongoni mwa mabanda aliyoyatembelea ni pamoja na banda la EPZA, NMB, CRDB, NBC, BOT kitengo cha mifumo ya malipo ya Kielektroniki ya Serikali, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na JKT.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, Waziri wa Ulinzi Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, Naibu Waziri Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Josephat Kandege, Naibu Waziri wa Madini, Stansalaus Nyongo pamoja na maafisa wengine wa Serikali.