Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abbas akizungumza na waandishi wa habari leo mara baada ya kutembelea mabanda katika maonesho ya 4 ya Wiki ya Viwanda kwa nchi za SADC yanayoendelea kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abbas akipata maelezo katika banda la Kagera Tea katika maonesho ya 4 ya wiki ya viwanda kwa nchi za SADC ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abbas akipata maelezo katika moja ya banda banda la linaloonesha vito mbalimbali katika maonesho ya 4 ya wiki ya viwanda kwa nchi za SADC ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
…………………………………………
NA JOHN BUKUKU
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abbas amesema ajenda kubwa ambayo Tanzania mara itakapochukua uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ni kusukuma mbele matumizi ya lugha ya Kiswahili kutumika katika nchi wanachama wa SADC.
Ameyasema hayo wakati akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari ambaye alitaka kujua nini serikali inafanya kuhusu lugha ya mawasiliano ambayo imeonekana kuwa tatizo kwa wajasiriamali wengi nchini na pia katika maonesho ya nne ya wiki ya viwanda ya SADC, yanayoendelea katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema Lugha ya Kiswahili inayozungumzwa sana katika nchi hizi ukiacha Kiingereza na Kireno lugha ambazo zilirithiwa kutoka kwa makoloni yaliyozitawala nchi hizo.
Ameongeza kwamba Lugha ya Kingereza inazungumzwa na nchi za Zambia, Malawi, Zimbabwe, Afrika Kusini na Namibia wakati nchi za Angola na Msumbiji zinatumia lugha ya Kireno ambazo pamoja na kuzizungumza haziwezi kutuunganisha pamoja kama jumuiya ya nchi za SADC.
Dk. Abbas ameongeza kuwa mpaka sasa Baraza la Kiswahili Tanzania limeshasajili zaidi ya wataalamu 1000 wa kufundisha kiswahili ambao wanaweza kupata fursa ya kufundisha Kiswahili katika mataifa mbalimbali ya nchi za jumuiya ya SADC.
“Nafasi bado zipo usajili huo unaendelea kama kwa wale wanaojua kuandika kiswahili , Kutafsiri au Kufundisha wanakaribishwa ili wajisajili kwa kuwa fursa ni nyingi na mahitaji ya wataalamu ni makubwa,” amesema Dk. Abbas.
Amesema Kama ilivyokuwa wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 4 wiki ya Viwanda kwa nchi za SADC jijini Dar es salaam Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipohutubia kwa kiswahili na kuzungumza na wataalamu wa sekta mbalimbali kutoka nchi za SADC na washiriki wa maonesho hayo
Walionesha kumsikiliza kwa makini kabisa na kwamba wanavutiwa na lugha ya kiswahili ambayo inaweza kutuunganisha zaidi kama jumuiya kuliko lugha zingine zinazotumika.