Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto), akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA, Bi. Dinah Edward, alipofanya ziara ya kikazi katika Mamlaka hiyo kubaini changamoto za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 na njia ya kuzitatua, katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto), akimsikiliza kwa makini Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA, Dkt. Edwin Mhede, kuhusu changamoto za Mamlaka hiyo hususani upungufu wa wafanyakazi wa kada mbalimbali takribani 2000, wakati wa mkutano katika Ofisi za Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam.
Mkutano kati ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA, Dkt. Edwin Mhede, ukiendelea katika Ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kulia), Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Christopher Nkupama (kushoto) na Mtaalam wa Sera wa Wizara hiyo Bw. Msabaha Msabaha, wakimsikiliza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA, Dkt. Edwin Mhede (hayupo pichani), alipokuwa akielezea mikakati ya ukusanyaji wa mapato.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto), akihoji masuala mbalimbali ya utekelezaji wa Bajeti, wakati wa mkutano kati yake na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA, Dkt. Edwin Mhede (kulia), alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi za Mamlaka hiyo, Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA, Bi. Dinah Edward (kushoto), akieleza changamoto za utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2018/19 wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (wa pili kushoto), jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (kulia) akiagana na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA, Bi. Dinah Edward, baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi katika Mamlaka ya hiyo, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam)
………………………
Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imejipanga kuongeza ufanisi wa kiutendaji na ukusanyaji wa Mapato wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA kwa kuongeza wafanyakazi na kuboresha makazi ya watumishi, ikiwa ni sehemu ya kutatua changamoto za utekelezaji wa Bajeti ya Mamlaka hiyo kwa mwaka wa Fedha 2018/19.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, wakati wa ziara ya kikazi ya kufuatilia mafanikio na changamoto za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Dkt. Kazungu alisema kuwa, amebaini upungufu wa takribani wafanyakazi 2000 wa kada mbalimbali katika mamlaka hiyo, hivyo kufifisha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa kiwango toshelevu ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Kama Wizara ya Fedha na Mipango tumeona kuna umuhimu wa kuiwezesha TRA katika rasilimali watu na fedha ili kuongeza mapato ya Serikali katika muda mfupi ujao ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla”, alieleza Dkt. Kazungu.
Alisema kuwa changamoto nyingine ni pamoja na upungufu wa vitendea kazi yakiwemo magari, ambapo ameahidi kulifanyia kazi suala hilo ili kurahisisha utendaji kazi wa Mamlaka hiyo muhimu katika mstakabali wa ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Dkt. Kazungu alisema ziara yake katika Mamlaka ya Mapato Tanzania ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara yake hususani katika eneo la changamoto zilizojitokeza kwa mwaka uliopita na kuangalia ni njia zipi zinaweza kutumika kuzitatua ili kuleta ufanisi kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu TRA, Dkt. Edwin Mhede, alimpongeza Dkt. Kazungu kwa kufanya ziara katika Taasisi yake na akamhakikishia kuwa amejipanga kimkakati kuhakikisha mapato yanaongezeka na pia iwapo suala la upungufu wa wafanyakazi litatatuliwa, ongezeko la makusanyo litakuwa sio jambo gumu kwa mamlaka yake.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatibu Kazungu, anafanya ziara katika Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha kubaini changamoto za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 na kuangalia utatuzi wake kwa mwaka wa fedha 2019/20.