Home Biashara MAUZO YA TOLEO LA TATU LA HATIFUNGANI ZA BENKI YA NMB YAWEKA...

MAUZO YA TOLEO LA TATU LA HATIFUNGANI ZA BENKI YA NMB YAWEKA HISTORIA KATIKA MAENDELEO YA MASOKO YA MITAJI

0
*CMSA yapeleka ujumbe kwa benki za biashara, wananchi kutumia fursa, DSE yagusia mafanikio ya NMB 
 
OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Nicodemus Mkama ametoa mwito kwa benki za biashara pamoja na benki za wananchi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya masoko ya mitaji ikiwemo kuuza hatifungani kwa umma na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa ili kuongeza mitaji yao.
 
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni muhimu kwani itasaidia utekelezaji wa agizo la Serikali kwa benki zote za biashara pamoja na benki za wananchi kutimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji wa kutosha ili kujiendesha kibiashara.
 
Mkama ameyasema hayo leo Agosti 2,2019 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la tatu la hatifungani ya Benki ya NMB katika Soko la Hisa Dar es Salaam ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa mauzo ya toleo la tatu la hatifungani ya benki ya NMB yameweka historia kubwa katika maendeleo ya masoko ya mitaji hapa nchini.
 
“Kwani mauzo haya yamekuwa na idadi na thamani kubwa kuliko mauzo yote ya hatifungani yaliyowahi kufanyika hapa nchini, ambapo jumla ya wawekezaji 2,264 wameweza kushiriki .Kati ya wawekezaji hao ,wawekezaji 2,253 ni wawekezaji wadogo sawa na asilimia 99.5 wakati wawekezaji 11 ni kampuni.
 
“Hatua hii ni muhimu kwani imewapatia fursa wawekezaji wadogo wadogo ambao ndio idadi kubwa ya wananchi kuwekeza katika masoko ya mitaji kupitia hatifunfani hii.Aidha kati ya wawekezaji hao , wawekezaji 1,381 wanatoka nje ya Jiji la Dar es Salaam , sawa na asilimia 61 ya wawekezaji wote.Idadi hii inajumuisha wawekezaji kutoka mikoa ya kanda zote nchini,”amesema.
 
Ameongeza kupitia mauzo hayo , masoko ya mitaji yamefanikiwa kupata wawekezaji wapya, ambapo kati ya wawekezaji 2,264, wawekezaji wapya ni 1,358, sawa na asilimia 60.Hatua hiyo ni muhimu kwani imeongeza idadi ya wawekezaji katika masoko ya mitaji na kuchangia utekelezaji wa mpango jumuishi wa huduma za kifedha hapa nchini.
 
“Fedha zilizopatikana kupitia mauzo hayo toleo hili zitatumika kugharamia shughuli za maendeleo ya benki ya NMB , ikiwa pamoja na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali pamoja na wawekezaji wadogo wadogo yenye lengo la kukuza na kuendeleza ujasiriamali nchini.
 
“Hatua hii ni muhimu kwani inatarajiwa kuwa na matokeo chanya katika ukuaji wa sekta binafsi na uchumi wa nchi kwa ujumla na hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuinua wananchi wenye kipato kidogo.Tunashukuru sana benki ya NMB kwa mikakati hii ya kuunga juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano,”amesema Mkama.
 
Pia amesema uorodheshwaji wa toleo la tatu la hatifungani ya NMB katika soko la hisa unawapatia fursa wawekezaji kuuza hatifungani zao pale wanapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine , kujua thamani halisi ya hatifungani zao na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hatifungani hizo ambapo wawekezaji hao hupata riba kama faida itokanayo na uwekezaji huo.
 
Mkama ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wadau wote wa masoko ya mitaji kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana katika kutekeleza mikakati ya kuendeleza masoko ya mitaji nchini ikiwemo kuleta bidhaa mpya katika masoko hayo ambazo zitaweza kuorodheshwa katika soko la hisa ili pamoja na mambo mengine kuwapatia wawekezaji taarifa mbalimbali kuhusu bidhaa hizo ikiwemo bei kwa namna iliyo wazi.
 
Kwa upande wake Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema “Leo tupo hapa kwa ajili ya tukio muhimu la kuorodheshwa hatifungani ya NMB ambayo tulipata idhini ya kuuza kwa wananchi yenye thamani ya Sh. bilioni 25.
 
“Leo hii tunafurahi kuwa hapa na wenzetu wa soko la hisa Dar es Salaam na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) kuorodhesha rasmi kwa asilimia 100 fedha zote tulizozipata kutokana na mauzo ya hatifungani ya NMB.Mauzo ya toleo la tatu la hatifungani ya benki ya NMB yalifunguliwa Juni 10 ,2019 na kufungwa Julai 8 ,2019 ambapo benki ya NMB ilifanikiwa kukusanya Sh.bilioni 83.3 ikilinganishwa na Sh.bilioni 25 zilizotarajiwa kukusanywa,”amesema.
 
Zaipuni amefafanua kwa taarifa tu hatifungani hiyo imepokea maombi 2264, kati ya maombi hayo ni maombi 14 tu ndio yamepita kwa madalali wa soko la hisa , maombi mengine 2250 wameyapokea kupitia matawi ya NMB na kwamba hilo ni jambo la kujivunia wao kama benki.
 
“Hii ni mara ya kwanza kwa hati fungani kupata mafanikio makubwa namna hii katika historia ya masoko ya mitaji nchini, hii inadhihirisha imani kubwa ya wawekezaji waliyonayo kwetu.Tunawashukuru Watanzania kwa kutuamini na kutuweka kuwa benki namba moja kwenye masoko ya mitaji,”amesema na kuongeza kwa niaba ya menejimenti ya NMB anatoa shukrani za dhati kwa taasisi zote zilizofanikisha uuzwaji wa toleo la tatu la hatifungani ya NMB.
 
Wakati huo huo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam(DSE) Moremi Marwa amesema anawapongeza NMB kwa mafanikio ya hali ya juu ambayo yamepatikana na ndio yamesababisha kuwepo kwa shughuli hiyo ya leo ya uoredheshwaji wa hatifungani ya NMB baada ya kuuzwa katika mnada wa awali ikiwa ni sehemu ya programu ya uuzaji wa hatifungani za benki hiyo ikiwa na thaman ya Sh.bilioni 200.
 
“Hatifungani ambayo tunairodhesha ni toleo la tatu katika programu hiyo ya Sh.bilioni 200.Katika hatufungani hii NMB walitarajia kupata Sh.bilioni 25 lakini makusanyo ambayo wameyapata ni mara tatu zaidi. Hivyo mafanikio hayo ni jambo kubwa na sio tu kwa NMB bali kwa wote walioko kwenye masoko ya mitaji na dhamana pamoja na sekta ya fedha kwa ujumla,”amesema.

OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Nicodemus Mkama akigonga kengele mbele ya Waandishi wa habari na Wageni waalikwa  kuashiria kufungua uuzaji wa Hisa,wakati wa hafla fupi ya kuorodheshwa kwa toleo la tatu la hatifungani ya Benki ya NMB katika Soko la Hisa Dar es Salaam,iliyofanyika jijini Dar Es Salaam.Pichani anaefuata ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam(DSE) Moremi Marwa ,Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna,Mwenyekiti wa Bodi benki ya NMB,Prof. Joseph Semboja na kushoto ni Ofisa wa Soko la Hisa Dar es Salaam,Emmanuel Nyalali.Picha na Michuzi Jr-Michuzi Media.

 OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Nicodemus Mkama akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa habari wakiwemo wageni waalikwa mbalimbali (hawapo pichani). waliofika kwenye hafla fupi ya kuorodheshwa kwa toleo la tatu la hatifungani ya Benki ya NMB katika Soko la Hisa Dar es Salaam, ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa mauzo ya toleo la tatu la hatifungani ya benki ya NMB yameweka historia kubwa katika maendeleo ya masoko ya mitaji hapa nchini.
 Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna akizungumza mbele ya Waandishi wa habari wakiwemo wageni waalikwa mbalimbali (hawapo pichani),waliofika kwenye hafla fupi ya kuorodheshwa kwa toleo la tatu la hatifungani ya Benki ya NMB katika Soko la Hisa Dar es Salaam,  “Leo hii tunafurahi kuwa hapa na wenzetu wa soko la hisa Dar es Salaam na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) kuorodhesha rasmi kwa asilimia 100 fedha zote tulizozipata kutokana na mauzo ya hatifungani ya NMB,amesema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam(DSE) Moremi Marwa akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari na Wageni waalikwa mbalimbali waliofika kwenye hafla hiyo,iliyofanyika leo jijini Dar es Salaa.Marwa amewapongeza NMB kwa mafanikio makubwa waliyoyapata 

“Hatifungani ambayo tunairodhesha ni toleo la tatu katika programu hiyo ya Sh.bilioni 200.Katika hatufungani hii NMB walitarajia kupata Sh.bilioni 25 lakini makusanyo ambayo wameyapata ni mara tatu zaidi. Hivyo mafanikio hayo ni jambo kubwa na sio tu kwa NMB bali kwa wote walioko kwenye masoko ya mitaji na dhamana pamoja na sekta ya fedha kwa ujumla,”amesema.

Wageni waalikwa mbalimbali  wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri kwenye hafla fupi ya kuorodheshwa kwa toleo la tatu la hatifungani ya Benki ya NMB katika Soko la Hisa Dar es Salaam,Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar. 

 Picha ya pamoja.