******************
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo,mkoani Pwani ,dkt Shukuru Kawambwa ameungana na wakazi wa Matumbini ,kata ya Makurunge, kumuangukia Rais.dkt John Magufuli ili kuwapatia hekta 12,000 zilizobaki katika eneo la RAZABA waweze kuishi na kufanya shughuli za kimaendeleo.
Aidha wameshtushwa kuona eneo hilo ambalo bado lipo mkononi mwa serikali huku upande wa ardhi ukiwa umemegwa na kupatiwa kanisa la KKKT ushirika wa Kimanga.
Kawambwa alimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,asikilize kilio hicho wakati alipokuwa katika ziara yake ya jimbo, Matumbini kata ya Makurunge ambapo wananchi walisema kero kubwa ni ukosefu wa ardhi ya makazi .
Alieleza, awali eneo hilo lilikuwa na hekta 55,000 ambayo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliipatia ranchi ya Zanzibar (RAZABA) kwa ajili ya ufugaji ng’ombe ambapo baadae ilishindwa kuendelea na shughuli hiyo.
Kawambwa alifafanua, kipindi cha Rais mstaafu Dkt.Jakaya Kikwete alifanikiwa kuzirejesha hekta 22,000 kati ya 55,000 na kupatiwa kampuni ya Eco Energy kwa ajili ya mradi wa miwa.
“Alipostaafu kikaingia kipindi cha awamu ya tano ,ambapo kilibaini Eco Energy nao wanasuasua na uendelezaji wa eneo hilo na kuamua kuhamisha umiliki huo na kupewa BAKHRESA hekta 10,000 kati ya 22,000 kwa ajili ya kiwanda cha sukari na kilimo cha miwa “
“Juhudi zilishafanyika miaka miwili sasa ,kwa kumuomba mkurugenzi aandike barua kwa waziri mwenye dhamana ,na alifanya hivyo kwa kuomba hekta 3,000 ,lakini sisi tunaomba huruma ya Rais, atupatie hekta zote 12,000 sawa na hekari 30,000 ili wananchi hawa waondokane na kero na mgogoro huu,alisisitiza Kawambwa.
Baadhi ya wakazi wa Matumbini akiwemo Mwanaharusi na Sp Kisura walisema ,Rais dkt Magufuli ni mtetezi wa wanyonge basi awaangalie na wao kwani wameteseka kipindi kirefu.
Walielezea, kutokana na kuishi eneo hilo kwa miaka mingi huku wakihamahama wanaendelea kuomba eneo lililobaki baada ya kumegwa kwa Bakhresa ili waishi kwa amani.
Sp Kisura alisema ,hawatambuliki, lakini cha kushangaza kuna kitongoji kiitwacho RAZABA na wakati wa uchaguzi ukifika hutakiwa kufanya uchaguzi ,hivyo ni vyema wakatambulika kwa kupatiwa ardhi hiyo.
Kwa upande wake ,mwenyekiti wa kamati ya mashamba KKKT ushirika wa Kimanga, aliwaambia wananchi kwamba,wao wamefuata taratibu zote hadi kwa waziri wa ardhi na wamepatiwa kihalali eneo hilo.
Ndipo mbunge wa jimbo hilo aliposimama tena,na kuwataka wasiendelee na shughuli zozote,waende ofisini kwake ili apate uhakika kwa waziri waliomtaja kwani eneo hilo lipo chini ya serikali.