NA EMMANUEL MBATILO
Mitandao ya Kijamii imekua kwa kasi ya ajabu sana kuanzia mwaka 2006 mpaka leo tofauti ni kubwa sana. Kuanzia Facebook, twitter, Instagram mpaka Youtube zimekuwa kwa kasi ya ajabu na kukusanya mamilioni ya watumiaji.
Kila kitu kina faida na hasara pia naweza kusema kuwa mitandao ya kijamii ina athari kubwa sana katika jamii, pia imeweza kurahisisha mambo mengi sana katika jamii yetu inategemea na mtumiaji anayetumia.
Zifuatazo ni baadhi ya Hasara za kutumia mitandao ya kijamii;
Kuvunjika kwa Maadili
Mitandao ya kijamii kama yalivyo maendeleo yoyote yameletwa na wazungu hivyo hasa kwa nchi zetu za Afrika zimeonja utandawazi wa hali ya juu ila sisi waafrika tuna mila na desturi zetu ambazo ziko tofauti na wazungu baadhi ya vitu vilivyoharibu maadili yetu ni ukiingia kwenye mtandao wowote wa kijamii utakutana na matusi yaliyopitiliza yaani lugha ambayo watu wanatumia. Pia vijana kufuata wanayofanya wazungu na kujiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, kupiga picha za uchi n.k.
Vijana wengine wakiwa bado wanaumri mdogo wanatumia mitandao ya kijamii kuanglia pivha za ngono ambazo ni hatari kwake.Hii inasababisha kuharibika kwa vijana wengi wenye umri mdogo.
Majanga na Vifo
Kupitia mitandao ya kijamii hasa facebook au Instagram watu wanakutana wanachati lakini hawajuani wanahisi mtu unayeongea naye ni mtu mzuri kuja kuonana wengi wanaishia kuuliwa au kubakwa.mfano mzuri hapa Tanzania tumeona na kusikia vijana wengi wanatekwa na kuuwawa ni baada ya kuonana kwenye mitandao ya kijamii na kuomba waonane na baadae majanga yanatokea.
Si kila mtu mwema hapa duniani, wengi hufanya biashara na matendo maovu ambayo yanasababisha kukatisha uhai wa mtu.Kuna wakati mwingine unatokea udanganyifu kwenye mitandao hii kwa kudanganywa kwa kuonyeshwa matukio ambayo si ya kweli na wengi kuamini hivyo na kusababisha majanga kwa baadhi ya watu.
Wizi na Utapeli
Kwa bahati mbaya mitandao ya kijamii inatumika vibaya sana tofauti na lengo au sababu zilizowekwa kuna watu wanatumia mitandao ya kijamii kuibia wengine yaani utapeli kwa kuuza vitu feki na kadhalika. Hivi karibuni kulitokea kukamatwa kwa baadhi ya watu wanaosadikika kuwa ni wezi wa mitandaoni, walikuwa wanawatumia ujumbe baadhi ya watu wakidai pesa na kusasbabisha watu wengi kutapeliwa.
Uzembe
Mitandao ya kijamii imesababisha uzembe na kujiendekeza kwa watu wengi hasa vijana wenye nguvu kabisa. Yaani hivi sasa kuna watu ambao watashinda kutoka asubuhi mpaka jioni kwenye facebook au instagram bila kufanya kazi yoyote yaani mtu ataamka asubuhi kabla hata ya kufanya kitu chochote aingie kwanza kwenye mitandao ya kijamii ndo asikie raha kitu ambacho hakileti maendelea yoyotekatika jamii, Tumeona na kusikia vijana wengi wanagombana na wazazi pamoja na walezi wao kwa sababu tu ya mitandao ya kijamii anaambiwa afanye hiki lakini anakaidi na kuendelea kutumia facebook au instagram na hata wengine wanafunzi wanashindwa kujisomea na kushinda muda wote kwenye mitandao ya kijamii.
Kuvunjika kwa Mahusiano
Kwa kiasi kikubwa mitandao ya kijamii imepelekea kwa mahusiano mengi sana kuvunjika yaani watu wengi wanaitumia vibaya hii mitandao, zamani ilikuwa ili upate mchepuko basi ukakutane na mtu mbali huko lakini siku hizi unakutana na mtu kwenye kiganja cha mkono wako hivyo imerahisisha zaidi watu kupata michepuko na kuvunjika kwa mahusiano mengi sana, hasa hawa wasichana wanaopiga picha za nusu uchi watu wanajikuta wanaharibu mahusiano yao. Kumekuwa na baadhi ya watu kupiga picha ambazo ni hatari kwenye mahusiano ya watu na kusababisha mahusiano au wanandoa wengi kuachana.
Ingawa Mitandao ya Kijamii ina faida nyingi hizi ni baadhi tu ya hasara za kuwepo kwa mitandao ya kijamii hasa kwa hizi nchi zetu za Afrika. Tujitahidi sana kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa sababu inatusaidia kugundua vitu vingi hasa mambo ambayo hatuyafahamu hasa kwa baadhi ya wanafunzi, saizi tumelaisishiwa kwenye hii mitandao unaweza kusoma kupitia mitandao ya kijami na hata kusoma kwa vitendo kwa kutumia youtube.