KATIBU Tawala wa wilaya ya Handeni Mwalimu Boniface Maiga akizungumza wakati wa utambulisho wa mradi wa kuhamasisha uwajibikaji wa jamii na mamlaka zinazohusika katika kuboresha elimu katika vijiji nane vya halmashauri ya wilaya hiyo uliokwenda sambamba na mkutano wa wadau uliofanyika Kata ya Mkata ambapo mradi huo unaendeshwa na asasi ya Tree of Hope chini ya ufadhili wa Foundation for civil Society (FCS) kulia ni Diwani wa Kata ya Mkata akifuatiwa na Mratibu wa Mradi wa Kuhamasisha uwajibikaji wa Jamii na Mamlaka zinazohusika katika kuboresha elimu kwenye vijiji nane Goodluck Malilo
Mratibu wa Mradi wa Kuhamasisha uwajibikaji wa Jamii na Mamlaka zinazohusika katika kuboresha elimu kwenye vijiji nane wilaya ya Handeni Goodluck Malilo akizungumza
Mratibu wa Mradi wa Kuhamasisha uwajibikaji wa Jamii na Mamlaka zinazohusika katika kuboresha elimu kwenye vijiji nane wilaya ya Handeni Goodluck Malilo kushoto akiteta jambo na Katibu Tawala wa wilaya ya Handeni Mwalimu Boniface Maiga mara baada ya kufungua
WATUMISHI wa Halmashauri wilayani Handeni mkoani Tanga wameonywa kuacha kufanya vitendo vya ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo zinazopelekwa kwenye maeneo yao kwani zitawatokea puani.
Hayo yalisemwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Handeni Mwalimu Boniface Maiga wakati wa utambulisho wa mradi wa kuhamasisha uwajibikaji wa jamii na mamlaka zinazohusika katika kuboresha elimu katika vijiji nane vya halmashauri ya wilaya hiyo.
Utambulisho huo ulikwenda sambamba na mkutano wa wadau uliofanyika Kata ya Mkata ambapo mradi huo unaendeshwa na asasi ya Tree of hope chini ya ufadhili wa Foundation for civil Society (FCS).
Alisema kwamba sio ambao watabainika wamehusika kwenye kufanya ubadhirifu wakifanya uchunguzi na wakibaini wamehusika watawashughulikia kwa mujibu wa sheria na hakuna ambaye atasalimika
Katibu Tawala huyo ambaye alimwakilisha Mkuu wa wilaya ya Handeni Godwin Gondwe alisema kwamba hawatakuwa tayari kuona fedha zinazopelekwa kwenye maeneo yao na serikali huku zikihujumiwa hivyo watakuwa wakali kwa kuhakikisha wahusika wanashughulikiwa.
“Niwaonye watumishi ambao mnaofanya ubadhirifu kwenye miradi inayotelekezwa kwenye maeneo yenu acheni tabia hiyo mara moja kwani hatutawavumilia na hili niseme kwamba fedha ya serikali hailiwi ni moto hivyo watakaobainika watashughulikiwa “Alisema.
Hata hivyo alisema kwamba wilaya hiyo imepokea milioni 362.5 kutoka Serikalini kwa ajili ya ukamilishaji na umaliziaji wa vyumba vya madarasa 29 vya shule ya msingi wilayani humo.
Fedha hizo zilitolewa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli ambaye amepania kuhakikisha wanafunzi wanasoma bila kuwepo kwa vikwazo vya aina yoyote ile.
Alisema kwamba bado ujenzi unaendelea kwa sehemu mbalimbali na haitafikia mwezi Agosti majengo hayo yatakuwa yamekamilika na hivyo kuondokana na changamoto zilizopo.
“Lakini pia niwapongeze Asasi ya Tree of hope kwa maana maeneo mradi huo umefanya kazi kuna mabadiliko makubwa ya uwazi na uwajibika lakini pia hata utoro umepungua kwa asilimia kubwa hivyo mradi huo umekuwa chachu kubwa sana kwa jamii “Alisema.
Awali akizungumza wakati wa mkutano huo wa wadau Mratibu wa Mradi wa Kuhamasisha uwajibikaji wa Jamii na Mamlaka zinazohusika katika kuboresha elimu kwenye vijiji nane Goodluck Malilo alisema kwamba mradi huo rasmi kutekelzwa na Asasi ya Tree of hope katika wilaya hiyo mwezi Agosti mwaka 2017 hdi Mwezi Julai 2018.
Alisema kwamba mradi huo ulikuwa ukitekelezwa kwenye vijiji vinne vya Halmashauri ya Handeni ambazo ni Michungwani (Kata ya Segera), Kwedizinga (Kata ya Kwedizinga), Kabuku Nje (Kata ya Kabuku) na Komsanga (kata ya Mgambo) chini ya ufadhili wa shirika la Foundation for Civil Society.
Malilo alisema baada ya utekelezaji wa mradi huo kwa awamu ya kwanza na kuonekana mafanikio makubwa asasi hiyo iliongezewa muda wa ufadhili kwa kipindi cha miezi mitano kuanzia Novemba mwaka 2018 hadi mwezi Machi 2019 ili kuendeleza kutatua changamoto za elimu katika vijiji hivyo.
Alisema kutokana na mafanikio ya mradi huo kuwa endelevu na yenye tija katika sekta ya elimu waliomba ufadhili kutoka Shirika la Foundation for Civil Society ili kutanua wigo wa maeneo ya utekelezaji kutoka vijiji vinne had inane ambapo walikubaliwa huku wakiongeza vijiji vya Mjani Mapana (Kabuku ndani),Hoza(Komkonga),Kitumbi (Kitumbi) na Mkata Mashariki (Mkata).
Hata hivyo alisema kwamba mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi nane kuanzia mwezi Julai 2019 hadi February 2020 huku akieleza shughuli za mradi zitakazotekelezwa katika vipindi viwili vya miezi minne minne .
Alisema shughuli hizo ni pamoja na mikutano ya wadau wa elimu,uundaji wa kamati za wananchi za uhamasishaji na ufuatiliaji uwajibikaji ,mafunzo ya utawala bora,midahalo ya wadau wa elimu,uhamasishaji uwajibikaji jamii na mamlaka husika katika kuboresha elimu ikiwemo utengenezaji na usambazaji wa vipeperushi vya uelimishaji ikifuatiwa na ziara za ufuatiliaji na tathimini katika maeneo ya mradi.
Mwisho