Mkuu wa mkoa wa Shinyanga , Bi Zainab Terak akiwa ameshika mpunga uliotokana na mbegu ya aina ya Supa BC iliyoboreshwa kwa Teknolojia ya Nyuklia kwa kutumia mionzi aina ya gamma iliyotumika kununurisha mbegu hizo mradi ulioofadhiliwa na Shirika la nguvu za Atomiki la kimatifa (IAEA) kwa kuratibiwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania(TAEC) kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Kilimo (SUA) na Taasisi ya Utafiti wa kilimo Zanzibar (ZARI) .
…………………
Wananchi wa Tanzania upande wa Zanzibar wameendelea kufaidika na mchele unaotokana na mbegu ya mpunga aina ya SUPA BC iliyoboreshwa kwa Teknolojia ya Nyuklia kwa kutumia Mionzi aina ya gamma iliyotumika kununurisha bengu hizo .
Mradi huo ulifadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) na kuratibiwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI) ili kuhakikisha mbegu hiyo inaboreshwa na kuwa yenye ubora wa hali ya juu.
Akizungumza katika maonesho ya nane nane yanayoendelea katika viwanja vya maonesho vya Nyakabindi, Wilayani Bariadi, Mkoani Simiyu, Mtafiti Msaidizi wa mazao ya kilimo katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar Bwana Hamza Hamid Hamza amesema kuwa mbegu hiyo ina ubora na huzalisha mpunga kwa wingi na kwa sasa ni chaguo la wakulima na wananchi wengi Kisiwani Zanzibar.
Amesema mbegu aina ya SUPA BC, ina uwezo wa kuzalisha mpunga hadi kufikia tani 7 kwa hekta moja ambapo huchukua muda wa siku 130 mpaka kuvunwa kwake hali ambayo kwa sasa imewahamasisha wakulima wengi kulima aina hiyo ya mpunga visiwani humo.
“Mchele unaotokana na mpunga wa mbegu ya SUPA BC ni mzuri, wenye harufu nzuri na wenye ladha tamu kwa walaji na wakulima wengi wanashawishika kupanda mbegu hiyo kwa wingi” alisema Hamza Hamid.
Kwa mujibu wa Hamza amesema kuwa mpunga huo una sifa nyingi ikiwemo urahisi katika kufikicha tofauti na mbegu nyingine nyingi za mpunga zilizozoeleka na kuwa mmea wake una urefu wa wastani na usioweza kuanguka baada ya kubeba mpunga ukiwa shambani hivyo hupelekea kubaki na mazao yote hadi wakati wa kuvuna pamoja na uwezo wa kutoa machipukizi mengi wakati wa ukuaji wake.
Mbegu hiyo ilizinduliwa rasmi na Wizara ya Kilimo na Mifugo ya Zanzibar mwaka 2011 ambapo mpaka sasa inaendelea kulimwa kwa wingi visiwani humo.
Mtaalamu huyo amesema kuwa teknolojia hii ya nyuklia kwa kutumia mionzi ya Gamma ikiendelea kutumika inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo hasa katika kutafiti wa mbegu mbali mbali za mazao hapa nchini.
Bw. Hamza pia ameshauri kwamba kwa sasa kutokana na mbegu hiyo ya mpunga kutumika visiwani Zanzibar pekee , ni wakati muafaka sasa mbegu hiyo ikaanza pia kutumika pia katika eneo la Tanzania Bara.