Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha vijana, Mhe Mariam Ditopile amempongeza Rais Dk John Magufuli kwa niaba ya vijana nchini kwa kuzidi kuondoa kero za usafiri.
Mhe Ditopile ametoa kauli hiyo baada ya jana Rais Magufuli kuzindua jengo la tatu (Terminal 3) la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amesema jengo hilo limeongeza hadhi ya uwanja huo na kwenda sawa na Uwekezaji ambao umekua ukifanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli.
” Tumeingiza ndege za kutosha na tunaendelea na Ujenzi mpya na ukarabati/upanuzi wa viwanja vya ndege, hii inaonesha jinsi gani Serikali yetu imejipanga katika kukuza uchumi wetu kupitia usafiri wa anga lakini pia uwezo wa ndege zetu kutua katika viwanja vikubwa vya kimataifa kunaongeza soko la watalii nchini,” amesema Mhe Ditopile.
Kuhusu usafiri wa Nchi kavu, Mbunge huyo amesema kuna barabara za kutosha na zenye ubora kwa zaidi ya asilimia 95 Nchi nzima na zimeunganishwa na mtandao wa lami.
” Ujenzi wa reli ya mwendo kasi/Treni ya umeme (SGR) unaendelea kwa kasi kubwa, Serikali inaenda kuwekeza ktk reli ya TAZARA*kwa kuboresha miundombinu pamoja na injini na mabehewa ya kutosha na ya kisasa kwa kushirikiana na wabia wenzetu jirani zetu wa Zambia,” amesema Mhe Ditopile.
Aidha amempongeza Rais Magufuli kwa namna anavyoendelea kukarabati vivuko na meli mbalimbali pamoja na kupanua na kuongeza bandari kavu.
” Kwa haya maendeleo makubwa yanayofanywa na Jemedari wetu Rais Magufuli hakika kunatupa deni kubwa sisi wasaidizi wake kuhakikisha tunawatumikia wananchi wanyonge kama ambavyo yeye mwenyewe Mhe Rais anafanya kwa vitendo,” amesema Mhe Ditopile.