Home Mchanganyiko WADAU WA NGOs WAITIKIA USAJILI KANDA YA KASKAZIN

WADAU WA NGOs WAITIKIA USAJILI KANDA YA KASKAZIN

0

Wanasheria kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu Maendeleo ya Jamii) wakitoa ushauri wa kisheria kwa baadhi ya wadau wa NGOs waliofika kwenye dawati la Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kukamilisha maombi ya usajili wa mashirika yao wakati wa zoezi la usajili wa mashirika hayo linaloendelea katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.

Afisa Maendeleo ya Jamie mkoa wa Kilimanjaro Bi. Hilda Lauwo Adios Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu Maendeleo ya Jamii) Victor Rugarabamu wakitoa ushauri kwa baadhi ya wadau wa NGOs waliofika kwenye dawati la Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kukamilisha maombi ya usajili wa mashirika yao wakati wa zoezi la usajili wa mashirika hayo linaloendelea katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.

 Wasajili wasaidizi kutoka Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA), Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (Usajili wa Asasai za Kiraia) na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini, RITA wakishiriki huduma ya pamoja ya msaada wa kisheria kwa baadhi ya wadau wa NGOs waliofika kwenye dawati kukamilisha usajili wa mashirika yao wakati wa zoezi la usajili wa mashirika hayo linaloendelea katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

…………………………………..

Wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambao awali walijisajili chini ya Sheria nyingine, wameendelea kuiitikia zoezi la usajili wa asasi zao katika siku ya tano ya usajili huo unaofanyika katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza na vyombo vya habari leo mkoani Kilimanjaro Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bw. Erasto Ching’oro ameeleza kuwa idadi ya wadau wanaofika kupata huduma ya usajili wa mashirika ya kijamii imepanda kutoka wastani wa mashirika 20 kwa siku katika siku mbili za kwanza hadi mashirika 35 katika siku ya tano likiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 75 ya wadau wanaofika kuhuisha usajili wao kwa mujibu wa mabadiliko ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Namba 3 ya mwaka 2019.

Bw. Erasto ameongeza kuwa, walengwa wakuu wa Usajili unaoendelea ni Mashirika naTaasisi zinayofanya kazi za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya jamii, ambao awali walisajiliwa chini ya Sheria nyingine ikiwemo Sheria ya Vyama  Sura 337, Sheria ya Udhamini Sura 375, na Sheria ya Makapuni Sura 212/213, kama zilivyofanyiwa mabadiliko na Sheria Namba 3 ya mwaka 2019, na sasa wanapashwa kusajiliwa chini ya Sheria stahiki ikiwemo Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Namba 24 ya mwaka 2019.

“Sheria hii inazitaka Mashirika yote zilizojisajili chini ya Sheria nyinginezo kuhakikisha kuwa zimekamilisha uhamisho wao ndani ya kipindi cha miezi miwili kuanzia siku ya tarehe 1 Julai, 2019 ili kuendelea kupata haki na hadhi ya kuendesha shughuli za katika jamii kwa kuzingatia sheria taratibu na kanuni.  Alisisitiza Bw.Erasto

Ameongeza kuwa mafanikio yaliyongeza mwitikio wa wananchi ni juhudi zinazofanywa na Ofisi za Wasajili wa Mamlaka husika  katika kuwajengea uelewa chanya kuhusu nia njema ya Serikali katika uendeshaji wa zoezi hili ambao unalenga kukuza mchango wa Mashirika hayo katika maendeleo na ustawi wa Watanzania.

Aidha Bw. Erasto ameongeza kuwa zoezi la kuhuisha usajili wa mashirika yanayofanya kazi za kijamii na kiuchumi katika ngazi ya jamii, wilaya, mkoa na Taifa linaumuhimu kwani litawezesha kuwa na matumizi bora ya rasilimali za nchi kwa kuwa na mtawanyiko wenye uwiano wa afua mbalimbali katika kuhudumia jamii, jamii itahamasishwa kuchangia maendeleo yao, itakuza ajira na weledi wa miradi na pia kukuza uwazi na uwajibikaji katika ngazi mbalimbali.

Usajili huu unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kisheria linaloelekeza Mashirika na Taasisi zote zinazofanya kazi za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya wananachi kuhakikisha kuwa yamekamilisha usajili wake chini ya Sheria Namba 24 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa mabadiliko chini ya Sheria Namba 3 ya mwaka 2019.

Kwa Kanda ya kaskazini zoezi hili la uhuishaji usajili limeanza tarehe 29 Julai 2019 na litahitimishwa tarehe 6 Agosti, 2019 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na linaendeshwa kwa utaratibu wa Kituo cha pamoja cha usajili ambacho kinajumuisha Msajili kutoka BRELA, RITA, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto(Idara kuu Maendeleo ya Jamii) kwa lengo la kutoa huduma katika sehemu moja na kuepuka urasimu.