Na Mussa John-Mara
Mkazi wa kijiji cha Kimusi wilayani Tarime mkoani Mara ameuwawa kwa kukatwa katwa mapanga na mtoto wake wa kuzaa na kisha mtoto huyo pia kuuwawa kwa kupigwa risasi na askari polisi waliofika katika eneo la tukio.
Akizungumza mjini hapa jana mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mara, kamanda wa polisi kanda maalum ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema kuwa tukio hilo lilitokea kijijini hapo Julai 29 saa 12 jioni na kumtaja mzee huyo kuwa ni Kisiri Nyambari (85)
Mwaibambe alisema kuwa muda huo kijana huyo aliyetambuliwa kwa jina la Wambura Kisiri (45-50) alitoka kwenye mji wake ulio jirani na mji wa baba yake mzazi akiwa na mapanga mawili mikononi na kufika kwenye mji wa baba yake ndipo alipoanza kumkata kata mapanga bila kuongea kitu chochote.
“Alimkataka shingoni, tumboni na kumkata mkono wake wa kushoto na kuutenganisha kabisa na mwili wake na yule mzee alifariki hapo hapo na akaendelea kuwajeruhi watu wengine akiwemo shangazi yake na ndugu wengine pamoja na majirani ambao hivi sasa wamelazwa katika kituo vha afya cha Murito” alisema Mwaibambe
Aliwataja watu waliojeruhiwa na kijana huyo katika tukio hilo kuwa ni Rhobi Nyambari (38) ambaye ni shangazi yake, Marwa Nyambari (28) ambaye ni baba yake mdogo na Chacha Mwikwabe ambaye ni jirani yao wote walijeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za miili yao.
Alifafanua kuwa baada ya polisi kupata taarifa walifika eneo la tukio na kujaribu kumkamata kijana huyo lakini ilishindikana kwavile alitishia kuwakata na mapanga hali iliyowalazimu kutumia mabomu ya machozi ambayo hata hivyo hayakusaidia.
Mwaibambe alisema kuwa kufuatia hali hiyo ilibidi polisi watumie risasi ambapo alipigwa kiunoni kisha kukamtwa lakini alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitalini.
Aliongeza kuwa hadi sasa chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika na kwamba polisi bado wanaendelea na uchunguzi huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Tarime ikisubiri taratibu za mazishi kutoka kwa ndugu na jamaa.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima alilitaka jeshi la polisi Tarime/ Rorya kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka ili.kujua chanzo cha tukio hilo ambalo alisema kuwa ni la kutisha.
” Hili tukio ni baya sana na linatisha hivyo naliagiza jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kama inawezekana tuweze kuzuia matukio kama haya yasitokee katika jamii yetu maana katika hali ya kawaida haiwezekani mtu umkatekate baba yako mzazi mapanga hadi utenganishe viungo na vya mwili huku ukiwajeruhi vibaya ndugu hadi majirani” alisema Malima.