Home Mchanganyiko Jumla ya wagonjwa 10 wenye matatizo ya umeme wa moyo ambao mapigo...

Jumla ya wagonjwa 10 wenye matatizo ya umeme wa moyo ambao mapigo yake yanadunda haraka kuliko kawaida na wengine yako chini ya asilimia 30 wamefanyiwa matibabu kwenye kambi maalum ya matibabu inayoendelea katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)

0

Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani
wakimwekea mgonjwa ambaye mapigo yake ya moyo yako chini kwa asilimia 25
kifaa maalum cha kuongeza utendaji kazi wa moyo (Cardiac resynchronization
therapy implantable cardioverter defibrillator – CRTD).

***********

Na Mwandishi Maalum

1/8/2019

Jumla ya wagonjwa 10 wenye matatizo ya umeme wa moyo ambao mapigo yake  yanadunda  haraka kuliko kawaida na wengine yako chini ya asilimia 30 wamefanyiwa matibabu kwenye kambi maalum ya matibabu inayoendelea katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Matibabu ya wagonjwa hao yamefanyika katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo Dkt. Peter Kisenge amesema kati ya wagonjwa 10 waliofanyiwa upasuaji katika kambi hiyo, wagonjwa wanne ambao mioyo yao ilikuwa imechoka na mapigo ya moyo kuwa chini ya asilimia 30 wamewekewa kifaa maalum cha kuongeza utendaji kazi wa moyo  kijulikanacho kwa jina la kitaalamu la “Cardiac Resynchronization Therapy implantable cardioverter Defibrillator” (CRTD).

Dkt. Kisenge aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza JKCI imeanza kuziba maeneo ambayo yanapitisha umeme wa moyo kwa wingi na kuleta shida katika moyo kwa kutumia mashine maalum (Electrophysiology machine) iliyotolewa hivi karibuni na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa ajili ya matibabu ya moyo hapa nchini.

“Mashine hii ya Electrophysiology inakazi ya kupima umeme wa moyo kama kuna mahali ambapo unapita bila kufuata njia ya kawaida pataonekana na baada ya hapo inatumika  kuziba njia hizo. Tatizo hili huwatokea zaidi wagonjwa wenye shinikizo la juu la moyo la  muda mrefu, wagonjwa wanaopata mstuko wa moyo, na wagonjwa wenye hitilafu ya umeme wa moyo katika  baadhi ya vyumba vya moyo,” alisema Dkt. Kisenge.

Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya moyo alisema matibabu ya kuziba maeneo yanapitisha umeme wa moyo bila kufuata njia yake  awali hayakuwepo hapa nchini hivyo kupelekea wagonjwa wenye shida hiyo kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu lakini kuanzia Julai 22 mwaka huu matibabu hayo yameanza kutolewa  hapa nchini.

Naye Mtaalamu wa mashine ya kuchunguza, kutathmini na kutibu umeme wa moyo unaoenda kwa haraka (Electrophysiologist) kutoka Shirika la Madaktari Afrika la Nchini Marekani Prof. Mathew Sachest alisema Madaktari Afrika wamekuwa wakishirikiana na madaktari wa JKCI kwa kipindi cha miaka mitatu sasa ambapo utoaji wa huduma za matibabu ya moyo umekuwa  kwa kasi ya hali ya juu hivyo kupunguza uhitaji wa wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Prof. Sachest alisema kupitia kambi maalum za matibabu wanazozifanya JKCI  madaktari , wauguzi na mafundi sanifu wa moyo wanapata  uzoefu wa kutoa huduma za matibabu zinazohitaji ujuzi wa hali ya juu na kuweza kutoa huduma hizo kwa wagonjwa.