Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Bashiru Taratibu akisema jambo wakati wa ufunguzi wa zoezi la utayari wa kukabiliana ana Ugonjwa wa Ebola kwa watoa huduma za afya Mkoani Kagera (hawapo pichani) jana Mjini Bukoba.
Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora akisema jambo wakati akifungua zoezi la utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola kwa Watoa huduma za afya katika Mkoa wa Kigoma (hawapo pichani) jana Mjini Bukoba.
Washiriki wa zoezi la utayari wa kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola kutoka Mkoa wa Kagera wakiwa kwenye majadiliano kuweka mikakati ya ugonjwa huo usiingie nchini.
Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani Dkt. Refeya Ndyamuba (aliyesamama) akisema jambo wakati wa ufunguzi wa zoezi la utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola nchini kwa watoa huduma za afya katika Mkoa wa Kigoma jana Mjini Bukoba.
Wataalam wa Afya katika Mkoa wa Kagera wakiwa katika zoezi la utayari wanajadiliana mikakati ya kudhibiti Ugonjwa wa Ebola usiingie nchini.
Picha ya Pamoja washiriki wa zoezi la utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola na Mgeni Rasmi, Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora (aliyeketi katikati).
…………………………………………………..
Na WAMJW – Bukoba, KAGERA
Watoa huduma za afya nchini wametakiwa kuweka juhudi madhubuti kuhakikisha Ugonjwa wa Ebola hauingii nchini Tanzania.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustinely Kamuzora alipokuwa akifungua zoezi la utayari jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa ebola kwa wataalam wa afya mkoani humo.
Akifungua zoezi la utayari, Profesa Kamuzora amesema “Tukifanya juhudi zetu za kukabiliana na ugonjwa wa ebola basi maisha yetu hayatokuwa hatarini” na kuendelea “Juhudi hizi zina matunda makubwa kuliko tukaruhusu ugonjwa huo kuingia nchini”
“Mpaka sasa hivi Mwenyezi Mungu ametujaalia hakuna mtu aliyeripotiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola nchini, tukifanya yale ambayo tunaelekezwa na wataalam wetu basi maisha yetu hayatokuwa hatarini” amesema Profesa Kamuzora.
Prof Kamuzola amewataka watoa huduma za afya kufuata taratibu zote zilizowekwa ili endapo ikitokea mtu akabainika kuwa na ugonjwa huo, basi aweze kupatiwa huduma na wakati huo huo mtoa huduma akawa salama.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Bashiru Taratibu amesema kuwa zoezi ya utayari lina lengo la kuzuia maafa yasitokee kwa kuwaweka tayari watalaam wa sekta ya afya kukabiliana na tishio la ugonjwa wa ebola kuingia nchini.
“Tuhakikishe tunazuia ugonjwa wa ebola usiingie nchini, na endapo ikitokea umeingia basi tuhakikishe tunapunguza athari zitokanazo na ugonjwa huo” amesema Bw. Taratibu.
Naye Mtaalam wa Afya ya Jamii na Masuala ya Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Faraja Msemwa amesema kuwa kupitia mazoezi hayo ya utayari wanapata fursa ya kubaini fursa na changamoto zilizopo katika kudhibiti ugonjwa huo wa ebola usiingie nchini.
“Katika zoezi hili tunaangalia hawa watumishi wetu wa afya tuliowandaa wana uwezo wa kiasi cha kuweza kufuata miongozo iliyoandaliwa” amesema Dkt. Msemwa.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) toka kuripitiwa kuibuka kwa ugonjwa wa ebola nchini Uganda mnamo mwezi Agosti mwaka 2018 jumla ya kesi 2612 za watu kuathiriwa na ugonjwa huo zimeripotiwa huku ukisababisha vifo 1756 (sawa na asilimia 67). Zoezi la utayari limepangwa kufanyika kuanzia leo JULAI 30 mpaka AGOSTI 8 mwaka 2019 ambapo vituo vya kutolea huduma za afya katika Mikoa ya Kagera na Kigoma vitapimwa utayari wao katika kukabiliana na Ugonjwa huo hatari.
Kupitia mazoezi ya utayari, watoa huduma za afya kuanzia ngazi ya jamii wanapata fursa ya kushiriki kwa vitendo namna ya kutambua, kutoa huduma kwa mtu anayehisiwa au kuwa na ugonjwa wa ebola na kuwaondolea woga pindi ikitokea mtu akabainika kuwa na ugonjwa huo.