MWENGE wa Uhuru,umezindua mradi wa tanki kubwa la maji linalojengwa Bagamoyo ,mkoani Pwani ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni sita linatarajiwa kuondoa tatizo la ukosefu wa maji kwa wakazi wa wilaya hiyo na maeneo jirani.
Baadhi ya wakazi wilayani hapo ,akiwemo Asia Rajabu na Ashura Selemani ,walielezea kero ya maji imepungua kama sio kubakia historia.
“Mradi huu ni mkombozi kwa sisi wananchi kipindi cha nyuma tulikuwa hatupati huduma ya maji safi na salama kwa uhakika,maana tulikuwa tunatumia visima vya kupampu na wakati mwingine vilikuwa vibovu,”
“Ilikuwa ni shida na kero maana tulikuwa tukikosa maji siku 5-7 ,lakini sasa tunashukuru mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA )na serikali kututua ndoo kichwani hasa sisi wanawake”walieleza.
Awali akimuelezea kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, juu ya mradi huo, meneja wa DAWASA Bagamoyo Alex Ngw’andu alisema katika hatua ya kwanza DAWASA wanatarajia kupata wateja 3,000 katika kata ya Ukuni,Sanzale,Nianjema na Kisutu ambapo hadi sasa wameshawaunganishia watu 250.
Alielezea kuwa, kata hizo zina watu 26,000 ambapo kila kaya itafikiwa hivyo waombe huduma waweze kusogezewa.
“Nia na madhumuni kupata mtandao wa kusambaza maji maeneo yote ya Bagamoyo na maeneo jirani”alisema Ngw’andu.
Akitoa maelekezo kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa ,Mzee Mkongea Ali aliwataka wamalizie maeneo ambayo hayajakamilika ili kufikia kila eneo asilimia 100 walizoziweka kwenye taarifa.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,Zainab Kawawa alisema mwenge wilayani hapo umepitia miradi 15 yenye thamani ya bilioni 4.370.