Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano PSSSF Unice Chiume akifungua semina ya Wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kuhusu mambo muhimu katika sheria ya PSSF namba 2 ya mwaka 2018 iliyofanyika jana katika jengo la Golden Jubilee Tower jijini Dar es salaam kutoka kulia ni Mwanasheria wa PSSSF Nicander Kileo na Ritha Ngalo Meneja wa PSSSF Temeke.
Victor Kikoti Meneja Matekelezo PSSSF akitoa akisisitiza jambo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya uwasilishaji wa mada katika semina hiyo katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano PSSSF Unice Chiume kulia ni Ritha Ngalo Meneja wa PSSSF Temeke.
Baadhi ya wahariri wa vyombo vya habri na waandishi wa habri wakifuatilia uwasilishaji wa mada katika semina hiyo.
Mwanasheria wa PSSSF Nicander Kileo akiwasilisha mada kuhusu Mambo muhimu katika sheria ya PSSSF namba 2 ya mwaka 2018 na kanuni zake.
Victor Kikoti Meneja Matekelezo PSSSF akiwasilisha mada ya Mwamko wa dhana ya Hifadhi ya Jamii Duniani wakati wa semina hiyo.
Kutoka kulia ni James Mlowe Meneja wa PSSSF Ilala, Unice Chiume Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano PSSSF, Ritha Ngalo Meneja wa PSSSF Temeke na Mwanasheria wa mfuko huo Mwanasheria wa PSSSF Nicander Kileo.
Afisa Habari wa PSSSF Abdul Njaidi na Eric Toroka wakifuatilia kwa makini mjadala katika semina hiyo.
Picha za pamoja mara baada ya semina hiyo.
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema umekusanya zaidi ya Sh.bilioni 1.7 kutokana na malimbikizo ya michango kutoka kwa waajiri 106 ambao walikuwa hawajawasilisha michango hiyo kwenye mfuko.
Mbali ya kukusanya fedha hizo ndani ya kipindi cha miezi nane, PSSSF imesisitiza umuhimu wa waajiri kuwasilisha michango kwa wakati ili kuepuka usumbufu huku ukitoa rai kwa watumishi kujiandaa kwa kuweka mazingira mazuri ya maisha wakati watakapostaafu utumishi wao.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam wakati wa semina ya wahariri na waandishi wa habari iliyoandaliwa na mfuko huo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu kufahamu mambo muhimu katika sheria ya PSSSF namba 2 ya mwaka 2018.
Wakati anatoa ufafanuzi kuhusu sheria, kanuni na taratibu za mfuko huo Mwanasheria wa PSSSF Nicander Kileo amesema kuna utaratibu mzuri uliowekwa katika kukusanya michango kwa waajiri na waajiriwa.
Hata hivyo kuna baadhi ya waajiri wamekuwa wakishindwa kuwasilisha michango kwa wakati na hivyo wamekuwa wakibanwa kwa sheria ikiwa pamoja ni pamoja na kufunguliwa kesi.
“Tunazo kesi 106 dhidi ya waajiri ambao wamechelewesha kuwasilisha michango ya wanachama .Kati ya kesi hizo 80 tumerithi kutoka kwenye mifuko mingine ya hifadhi ya jamii ambayo imeunganishwa kwenye mfuko wetu.Hivyo kupitia kesi hizo tumewabana waajiri hao na ndani ya miezi nane tumekusanya Sh.bilioni 1.7.
“Tumeweka utaratibu inapofunguliwa kesi, kabla ya muajiri husika kuanza kujieleza anatakiwa kutanguliza fedha za michango anayodaiwa na baada ya hapo sasa ndio anasikilizwa kama ana utetezi wa aina yoyote,”amesema.
Kwa upande wake Meneje Matekelezo wa PSSSF Victor Kikoti yeye aliwasilisha mada ya Mwamko wa dhana ya hifadhi ya jamii duniani na Mafao ya hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma ambapo ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha watumishi umuhimu wa kujiandaa kustaafu tangu siku ya kwanza wanapoajiriwa.
“Kuna umuhimu mkubwa kwa watumishi wa umma kutambua kuna maisha ya kustaafu baada ya kufanya kazi.Hivyo lazima kuwa na maandalizi mapema na kukumbuka licha ya leo kuwa kazini , kesho kuna kustaafu.
“Watumishi wengi wanajisahau na kuona kana kwamba hakuna kustaafu na matokeo yake wakiandikiwa barua ya kukumbushwa kumaliza utumishi wao wengine wanajikuta kwenye wakati mgumu kwani wanakuwa hawakujiandaa.Hivyo jukumu letu ni kuwakumbusha kuwa leo mko kazini lakini kuna siku mtastaafu kwa mujibu wa sheria,”amesema Kikoti.
Amefafanua zaidi kwenye hilo lazima mtumishi ajipange na kujiuliza maswali kadhaa ambayo ni ya kawaida, lazima ajiulize kwa muda wake wa utumishi alionao amefanya mambo gani ya maendeleo.Pia anaweza kujiuliza atakapostaafu anataka kwenda kuishi wapi.
Wakati huo huo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano PSSSF Unice Chiume amezungumzia sababu za kuandaa semina hiyo ambapo amefafanua wanahitaji kutoa elimu ya kutosha na ya kina kuhusu mfuko huo kwa waandishi wa habari ambao ni daraja kati yao na watumishi na waajiri.