Sehemu ya umati wa wananchi wa kijiji cha Kalemawe wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, wakishuhudia tukio la kuwashwa rasmi umeme katika kijiji hicho. Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) aliwasha umeme katika Zahanati ya Kijiji hicho, Julai 30, 2019.
Umati wa wanafunzi na walimu wa shule ya sekondari Kihurio iliyopo wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro wakishuhudia tukio la kuwashwa umeme katika shule hiyo. Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), aliwasha umeme katika shule hiyo, Julai 30, 2019.
Na Veronica Simba – Kilimanjaro
Serikali imesema kipaumbele cha kupeleka umeme vijijini ni kwa taasisi za umma pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo inayohudumia wananchi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliyasema hayo kwa nyakati tofauti, jana Julai 30 akiwa katika ziara ya kazi wilayani Same na Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kalemawe, wilayani Same, muda mfupi baada ya kuwasha rasmi umeme, Waziri aliwasisitiza viongozi wa taasisi na miradi mbalimbali ya umma kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ili huduma hiyo ipelekwe katika taasisi zao badala ya kuendelea kulalamika pasipo kuchukua hatua.
“Niwaambie ukweli ndugu zangu; kuanzia sasa sitaruhusu kiongozi wa taasisi au mradi wa umma kusimama na kulalamika kuwa taasisi yake haina umeme, wakati yeye mwenyewe hajalipia huduma hiyo. Sitampa nafasi. Lipieni ndipo mdai umeme.”
Akifafanua zaidi, Waziri Kalemani alisema kuwa, kutokana na umuhimu wa taasisi za umma kuwa na umeme, Wizara yake imeweka mkakati wa kupeleka huduma hiyo kwenye taasisi yoyote iliyolipia pasipo kujali umbali ilipo.
“Hata kama haiko kwenye mpango wa kupelekewa umeme kwa wakati huo; ilimradi imelipiwa, tutaifuata na kuiunganishia.”
Aidha, Waziri Kalemani aliwaambia wanafunzi wa shule ya sekondari Kihurio wilayani Same, wautumie umeme ambao serikali imewapelekea, kuboresha zaidi kiwango cha ufaulu.
Kwa upande wa waalimu, aliwataka kuutumia umeme huo kufanya maandalizi ya kufundisha vema zaidi lakini pia kwa maendeleo yao binafsi.
Katika ziara hiyo, Waziri pia aliwasha umeme katika kijiji cha Kigonigoni, wilayani Mwanga ambapo aliwahamasisha wananchi ambao hawajaunganishiwa umeme, kuondokana na kasumba ya kujidharau kuwa hawastahili kuunganishiwa umeme kutokana na aina ya makazi waliyonayo.
“Ndugu zangu, Rais Magufuli ametuagiza tuwaunganishie umeme wananchi wote pasipo kujali aina ya makazi waliyonayo, hivyo nanyi muache kujibagua. Umeme hauchagui nyumba. Tafadhali lipieni shilingi 27,000 ili muunganishiwe,” alisisitiza.
Awali, akiwasilisha kwa Waziri taarifa ya utendaji kazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Kilimanjaro, Meneja husika, Mhandisi Mahawa Mkaka, alisema hali ya usambazaji umeme mkoani humo imeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini na miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo.
Alisema, mpaka sasa vijiji 453 kati ya 519 vimeshapelekewa umeme ambapo ni sawa na asilimia 87.28 na kwamba, matarajio ni kufikia vijiji 493 sawa na asilimia 95 ifikapo Desemba, 2019.
Kwa upande wao, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Same, Anna Kilango Malecela na Mbunge wa Mwanga (CCM), Jumanne Maghembe, kwa nyakati tofauti waliipongeza serikali kupitia Wizara ya Nishati, kutokana na kazi nzuri inayofanyika, kupeleka umeme katika maeneo ambayo hayakutarajiwa, hususan kwa wananchi walioko vijijini.
Waziri amekamilisha ziara yake mkoani Kilimanjaro na ataendelea na ziara hiyo katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.