Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimkabidhi zawadi Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Watu wa China Bw. Li Bin katika hafla ya uzinduzi wa kambi ya matibabu na upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Jakaya Kikwete mapema leo jijini Dar Es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akipokea zawadi kutoka kwa mgeni wake Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Watu wa China wakati walipozindua Kambi ya matibabu na upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Jakaya Kikwete Jijini Dar Es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Waziri wa Afya wa China Bw. Li Bin (waliosimama) wakishuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya kambi ya upasuaji na matibabu ya moyo katika Taasisi ya Jakaya Kikwete yatayoratibiwa kwa ushirikiano wa madaktari wa JKCI na wa jimbo la Shadong nchini China. Kushoto anayesaini ni Prof. Mohamed Janabi na kulia ni mwakilishi kutoka Shadong.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea katika uzinduzi wa kambi ya matibabu na upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Jakaya Kikwete Jijini Dar Es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Kulia) akiwa na Waziri wa Afya wa China Bw. Li Bin wakifuatilia maelezo ya daktari (hayupo pichani) wakati walipotembelea chumba cha uangalizi maalumu kwa wagonjwa wa moyo kilichopo taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar Es Salaam.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiwa na mtoto aliyelazwa katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete wakati alipotembelea baadhi ya wodi ili kuona hali ya huduma za matibabu zinazotolewa kwenye taasisi hiyo kabla ya uzinduzi wa kambi ya matibabu na upasuaji wa moyo mapema leo.
……………………….
Na WAMJW-DSM
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Jamhuri ya watu wa China imezindua kambi ya huduma za hali ya juu za upasuaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wenye matatizo hayo.
Kambi hiyo imezinduliwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kwa kushirikiana na Naibu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya watu wa China Bw. Li Bin ili kutoa huduma za matibabu ya moyo pamoja na upasuaji lengo likiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kufuata huduma hizi.
“Kupitia kambi hii Watanzania watapata huduma za hali ya juu za upasuaji na matibabu ya moyo, itatusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya huduma hizi, pia kambi itatoa mafunzo ya juu katika ujuzi wa kisasa kwenye upasuaji na Tiba ya moyo kwa wataalamu wetu kwa kushirikiana na madaktari kutoka jimbo la Shadong”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema tatizo la magonjwa yasiyoambukizwa Tanzania na duniani kote limeongezeka kwa kasi ambapo takwimu za sasa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha ukubwa wa tatizo hili kuwa takribani watu Milioni 17 hupoteza maisha kila mwaka ikiwa ni sawa na asilimia 60 ya vifo vyote huku akiongeza kuwa vifo hivyo asilimia kubwa vinatokea katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa sababu kuu ya maradhi ya moyo nchini kama zilivyo nchi nyingine za kiafrika ni homa ya Rumatiki (Rheumatic Fever). Hivyo inakisiwa kuna watoto kuanzia asilimia 1.7-15 kati ya watoto 1000 wa shule waliobalehe wana ugonjwa huu.
Waziri Ummy ametaja sababu nyingine ya magonjwa ya moyo kuwa ni ya kurithi au kuzaliwa nayo kwa asilimia 0.35, ikimaanisha kuwa kuna takribani watoto 5000 wanaozaliwa na magonjwa ya moyo ya kurithi na karibu asilimia 50 wanahitaji upasuaji ili kurekebisha kasoro zilizopo katika mioyo yao kwa mwaka.
Hata hivyo, Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya China katika kupunguza mzigo wa maradhi haya nchini kufuatia kuanzishwa kwa Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete na sasa timu bora ya madaktari wa moyo kutoka jimbo la Shadong imekuja kutoa huduma katika kambi ya upasuaji na matibabu ya moyo inayoendelea katika taasisi hiyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya wa China Bw. Li Bin amesema Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha huduma za sekta ya afya nchini ikiwa ni kuenzi ushirikiano ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo. Serikali ya China imesaidia kujenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kupitia Rais wa zamani wa nchi hiyo Mh. Hu Jintao na jiwe la msingi liliwekwa mwezi Machi mwaka 2010 na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.