Mmoja kati ya wakurugenzi wa asasi ya Mirerani Tanzanite Mining Tourism ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Nuru Mkirery akizungumza kwenye mafunzo ya ujasiriamali.
Mmoja kati ya wakurugenzi wa asasi ya Mirerani Tanzanite Mining Tourism, Charles Mnyalu akizungumza katika semina hiyo.
………………….
WAJASIRIAMALI 50 wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kuwa wabunifu kwa kuandaa vitu vitakavyokuwa endelevu kwa jamii na siyo kupoteza muda kwa kuiga biashara zisizo na tija.
Mtaalamu wa saikolojia wa jijini Arusha, Joseph Mrindoko aliyasema hayo wakati akiwajengea uwezo wajasiriamali hao 50 kwenye ukumbi wa Mazubu Grand Hotel mji mdogo wa Mirerani.
Mrindoko alisema wajasiriamali wanapaswa kutambua kuwa wanatakiwa kufanya kazi kupitia maono ya mioyo yao tangu utotoni kwani ndiyo watapata mafanikio.
Alisema kanuni za maisha zinaeleza kuwa usipofanya chochote hautapata chochote na kadiri unavyofanya ndiyo utakavyopata hivyo wasibweteke kwenye maisha yao.
“Akili ya binadamu ina sehemu tatu tuzitumie zote na ukiwa duniani hakikisha unaacha alama tusilale mchana mfano mimi huu mwaka wangu wa nane nalala kwa muda wa saa nne pekee kwa siku na wala sijaugua ugonjwa wowote,” alisema Mrindoko.
Mmoja kati ya wakurugenzi wa asasi ya Mirerani Tanzanite Mining Tourism, Charles Mnyalu alisema kupitia mafunzo hayo wajasiriamali hao wataongeza uelewa ili wajinufaishe wao wenyewe na jamii kwa ujumla.
Mnyalu alisema wao kama Mirerani Tanzanite Mining Tourism wamedhamini mafunzo hayo kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kuwanyanyua kiuchumi wajasiriamali hao pindi wakizingatia elimu waliyoipata.
Mkurugenzi mwenza wa asasi hiyo Nuru Mkirery alisema mafunzo hayo yametolewa bila malipo kwa lengo la kuwajali wajasiriamali hao ili wachangamkie fursa mbalimbali zilizopo.
“Mwalimu Mrindoko amewafundisha wajasiriamali hawa watoke kwenye duara walilopo na kufikiria nje ya hapo kwani binadamu akitumia akili aliyonayo ambayo ni rasilimali aliyonayo anaweza kunufaika maishani mwake,” alisema Mkirery.
Mmoja kati ya wajasiriamali walioshiriki mafunzo hayo Hamis Seif alisema yeye anatengeneza na kuuza mabegi na amefaidika kwa elimu hiyo ikiwemo kuwekeza kwenye muda na kusimamisha jua.
“Katika mafunzo haya nimejifunza pia umuhimu wa kuwa mtanashati kwani mara nyingi watu wanakihukumu kitabu kutokana na muonekano wa jalada lake na siyo kurasa zilizo ndani yake hivyo tunapaswa kubadilika,” alisema.
Mjasiriamali wa mboga Zainabu Mussa alisema amefaidika na mafunzo hayo kwa kutakiwa kuwajali wateja na kuthamini biashara yake ikiwemo kuiboresha kwa kuwafikishia majumbani kuliko kuwasubiri gengeni.