*************
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2019 ,Mzee Mkongea Ali amenusa ubadhilifu wa fedha, katika mradi wa maji Ikwiriri huko Rufiji ambao umejengwa na mamlaka ya maji safi Dar es salaam DAWASA kwa zaidi ya sh.bilioni 2.055.6.
Kufuatia shaka hiyo, Mkongea amemuagiza kamanda wa TAKUKURU wilayani hapo kukamilisha agizo hilo ndani ya wiki mbili, kisha kupeleka taarifa TAKUKURU makao makuu na nakala itumwe kwake ili kama kutabainika uchakachuaji hatua ziweze kuchukuliwa.
Alitoa agizo hilo wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea mradi huo na kubaini baadhi ya dosari na kukosa nyaraka muhimu zilizotumika katika manunuzi ya baadhi ya vifaa.
“Tunapotembelea miradi hii tunahitaji kupata taarifa kamili za mradi ,tumetembelea hapa na kutoonekana nyaraka mbalimbali,huku tukimuuliza mtaalamu kuhusiana na fedha na matumizi yaliyoainishwa lakini hana majibu na kudai vitu vingine havipo”
“Hili suala la matanki manne ya jengo ambayo yalitengewe kiasi cha sh milioni 64 .5,vifaa vilivyotumika wakati wa survey milioni 5 tumeomba taarifa za mchanganuo hamna,mtaalamu ameulizwa anasema havipo,fedha zilizotengwa kwa ajili ya zege ,kokoto ,mchanga laki tano ofisa wa TAKUKURU kachunguze hili na nakukabidhi taarifa za mradi ili kuendelea na kazi ya ufuatiliaji”alifafanua Mkongea.
Mkongea alimkabidhi nyaraka zinazoonyesha taarifa za mradi kwenda kuchunguza kwa kina baada ya wao kupitia kwa muda mchache na kunusa ubadhilifu huo.
Nae mkuu wa wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo alimuhakikishia kiongozi huyo wa mbio za mwenge kuwa atalisimamia suala hilo.
Alieleza, kabla ya mwenge kuanza ziara hiyo viongozi wa wilaya hiyo walishiriki kikao cha kamati ya sherehe ambacho kiliitishwa na mkuu wa mkoa mhandisi Evarist Ndikilo na kuagiza kwamba wataalamu kutoka DAWASA kuwepo katika miradi yote ya maji itakayopitiwa na mwenge lakini cha kustaajabisha wataalamu hao hawakutokea katika mradi huo.
Wakati huo huo akipokea taarifa ya uchaguzi wa serikali za mitaa kijiji cha Kilimani ,Mkongea aliwataka wananchi kuchagua viongozi bora wasiopenda rushwa bali wawe wale watakaoleta mabadiliko ya nchi.
Aliwaomba wasirubunike na viongozi wanaopenda madaraka kwa kushawishi rushwa kwani kura moja italeta mabadiliko hivyo wasikubali kununuliwa wachague viongozi walio bora na si bora kiongozi.
Awali Njwayo alibainisha, mwenge wa uhuru ukiwa wilayani Rufiji umepitia miradi tisa yenye thamani ya sh.bilioni 2.562 .