**************
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro
KATIBU mkuu wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe amefanya ziara katika Mradi wa kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga-ERPP) unaotekelezwa katika Wilaya za Kilosa, Kilombero na Mvomero Mkoani Morogoro na kutorishwa na kasi ya wakandarasi katika ujenzi wa Maghala ya kuhifadhia Mpunga.
Mradi wa ERPP unatekelezwa na Wizara ya Kilimo ukiwa na lengo la kuongeza tija katika uzalisha wa zao la Mpunga kwa kutoa mbegu bora za zao hilo, ukarabati wa skimu za umwagiliaji ujenzi wa Maghala pamoja na utafutaji wa masoko.
Aidha Mradi wa ERPP unatekelezwa katika Visiwa vya Zanzibar huku Tanzania Bara ukitekelezwa katika Maeneo matano ya Mkoa huo.
Akiwa katika ziara hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe ametembelea ujenzi wa Maghala katika Kijiji cha Mvuha Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ghala la Kijiji cha Msolo ujamaa Kilombero, Kijiji cha Njage Kilombero pamoja maghala ya Kijiji cha Kigugu na Mbogo katika Halmashauri ya Wilaya Mvomero.
Mhandisi Mtigumwe amesema kuwa serikali haitosita kuwachukulia hatua wakandarasi hao kwa kuchewesha kazi wanazopatiwa pasina kuwa na sababu za msingi.
Amesema kuwa hatua zitakazochuliwa ni pamoja kupeleka mapendekezo katika bodi za wakandarasi ili kampuni hizo ziweze kufutiwa usajili nchini kutokana na kutotimiza matakwa ya serikali katika ujenzi wa maghala hayo ikiwemo kutokukabidhi kazi kwa wakati pamoja na ujenzi chini ya Kiwango.
Awali Viongozi wanaosimami mradi huo katika Mkoa wa Morogoro walimueleza katibu Mkuu wa Kilimo kuwa Baadhi wa wakandarasi wamekuwa wazito katika ujenzi hali inayotia wasiwasi wa kushindwa kukabidhi kazi kwa wakati.
Nao Baadhi ya wananchi wakizungumza kwa nyakati tofauti wameishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo na kueleza kuwa utakuwa chachu ya kuongeza uzalisha wa zao la Mpunga hali itakayofanya waweze kuongeza pato lao pamoja na kuchangia uchumi wa Taifa
kwa Upande wao wakandarasi hao wamesema kuwa awali walikuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali huku pia wakimuahidi katibu Mkuu huyo kukamilisha kazi kwa wakati na kiwango kinachotakiwa na serikali.