Home Mchanganyiko BANDARI YA KISASA KUFUNGUA LANGO LA BIASHARA KATAVI

BANDARI YA KISASA KUFUNGUA LANGO LA BIASHARA KATAVI

0

Sehemu ya eneo itakapojengwa Bandari ya Kisasa ya Karema wilayani Tanganyika

Baadhi ya viongozi wa CCM mkoa wa Katavi na watumishi wa serikali wakiwa na Balozi Silima katika ufukwe wa Ziwa Tanganyika

Sehemu ya Ziwa Tanganyika likionekana likiwa limetulia

*************

Na Mwandishi wetu, Katavi

Mradi wa ujenzi wa bandari ya kisasa utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 65 katika kata ya Karema wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi utawezesha kufungua lango kuu la biashara kati ya mkoa huo na nchi jirani ya Kongo DRC kutokana na nchi hiyo kutegemea chakula kutoka mkoani katavi ambapo kwa sasa kinasafirishwa kwa kutumia majahazi

Akizungumza na Wanahabari Katibu tarafa wa tarafa ya Karema Bi. Zawadi Mirambo,amesema kuwa tayari wametenga eneo la ukubwa wa mita 1000 kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo hivyo mita 500 ni kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo na mita nyingine 500 ni ziada itakayoendelezwa baadae ambapo wananchi waliopo katika eneo hilo wapo tayari kupisha mradi mara watakapolipwa fidia.

Naye Afisa Tawala wa wilaya ya Tanganyika Bwana Reginald Mhango amesema tayari serikali imekwisha idhinisha kiasi cha shilingi bilioni 25 kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi huo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini Bw. Selemani Kakoso amesema bandari hiyo ya kisasa itaboresha uchumi wa watu wa Katavi na nchi kwa ujumla kutokana na upande wa Kongo Kusini kupokea kiasi kikubwa cha chakula kutoka mkoani Katavi.

“Si Mahindi na Mchele tu hata Kitunguu wanachopikia Kongo kinatoka Katavi”. Amesema mbunge huyo.

Katibu wa Halmashauri kuu ya Taifa Bw. Pereira Silima ambaye pia ni mlezi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Katavi amefika kukagua eneo itakapojengwa bandari hiyo ambapo amewataka viongozi kuwa makini katika usimamizi wa utoaji wa fidia kwa wananchi na usimamizi wa mradi wenyewe.