Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na wananchi wa Kata ya Nansimo, Mwibara, Wilayani Bunda, Mara, leo, ambapo amesema Serikali itayafuta makampuni ya ulinzi binafsi nchini ambayo yanaajiri askari vikongwe, wasiokuwa na mafunzo ya askari wa akiba (mgambo) wala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), na kutowalipa au kuwalipa mishahara midogo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Isack Mahela.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na wananchi wa Kata ya Chitengule, Mwibara, Wilayani Bunda, Mara, leo, wakati alipokuwa anakagua ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Chitengule jimboni humo. Lugola aliwataka wananchi hao kufanya kazi kwa kujitolea na sio kuwa na Imani kula kila kitu kinafanywa na Serikali. Aliyevaa Kaunda suti ni ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Isack Mahela. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
……………………………………………………
Na Felix Mwagara, Mwibara (MOHA)
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Serikali itayafuta makampuni ya ulinzi binafsi nchini ambayo yanaajiri askari vikongwe pamoja na wasiokuwa na mafunzo ya askari wa akiba (mgambo) wala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Lugola amesema Wizara yake haiwezi kucheza na masuala ya ulinzi na usalama wa nchi kwa kuyaacha makampuni hayo yakiendelea kuajiri vikongwe ambao hawezi kushika silaha za moto na pia mara kwa mara wanasinzia kiasi kwamba muda wowote wanaweza wakanyang’anywa silaha na majambazi ambao wanazitafuta silaha kwa ajili ya kufanyia uhalifu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa Kata ya Nansimo, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda Mkoani Mara, leo, Lugola amesema kutokana na upungufu wa askari, Serikali iliruhusu kuwepo na makampuni binafsi ya ulinzi kwa ajili ya kusaidia masuala ya ulinzi na usalama nchini, lakini baadhi ya makampuni hayo yanavunja sheria kwa kuajiri walinzi wasiokuwa na mafunzo yoyote, askari waliostaafu ambao wamechoka na hawawezi kufanya kazi hizo na pia wanalipwa mishahara midogo au kutokulipwa kabisa.
Amesema kwa miaka ya hivi karibuni Serikali imeendelea kuwa na utaratibu wa kuhakikisha kwamba kwa wale wanaopita katika Jeshi la Akiba ambao wanaitwa Mgambo, na wale wanaopitia katika Jeshi la Kujenga Taifa, maeneo hayo mawili yasaidie kuzalisha askari ambao watachukuliwa na Makampani ya Ulinzi ili waweze kufanya kazi kwasababu wanauzoefu wamefundishika, wanajua jinsi ya kubeba na kutumia silaha za moto, namna ya kufanya doria pamoja na kulinda mali na maisha ya wananchi.
“Lakini niendelee kusikitika, baadhi ya makampuni, tumeshuhudia, yanaendelea kuajiri askari ambao wamechoka, askari ambao wamestaafu kwa mujibu wa umri wao, kwa maana hawawezi kufanya kazi tena hizi za kiaskari, lakini wanaajiriwa tena katika makampuni haya ya ulinzi, lakini pia tumeshuhudia unashtukia tu asubuhi mwananchi uliyemuona jana mtaani, na unamjua kabisa huyu mtoto wa fulani, hana mafunzo yoyote ya askari wa akiba, hana mafunzi yoyote ya Jeshi la Kujenga Taifa, ambapo vijana wanafundishwa uzalendo, uadilifu, lakini unamuona ghafla amebeba bunduki, amevaa sare za kampuni ya ulinzi, ana kirungu na anasema mimi nimepata ajira pale mjomba kanipeleka,” alisema Lugola.
Amesema yeye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, na kupitia Jeshi la Polisi nchini, haiwezekani masuala ya ulinzi na usalama ukachezewa, ambapo Ulinzi unahitajhi watu wenye mafunzo, watu wakakamavu, watu ambao hawana maradhi, na pia unahitaji watu ambao wanaweza wakafukuzana na uhalifu lakini baadhi ya makampuni hayo yanaajiri watu ambao hawana sifa hizo.
Lugola alisema, kutokana na changamoto hiyo, Serikali inakaribia kukamilisha kuwepo na sheria ya makampuni hayo ya ulinzi, ambayo itasimamia vizuri makampuni yote nchini, na sheria hiyo itaenda kudhibiti pia masuala ya ajira askari hao.
“Unaona mzee anatoka kazini asubuhi na bunduki yake kachoka hatua ishirini tu ameona mti pale kuna kivuli anafika hapo anaanza kusinzia mzee wa watu na bunduki, hata yunifomu zenyewe hazimkai vizuri, kachokaa, eti huyo ni askari wa kampuni binafsi ya ulinzi, haiwezekani, silaha hizi zinahitaji umakini katika kubeba na katika kutumia, na wahalifu nao wanazitafuta silaha za namna hii, wakigundua mahala fulani kuna walioajiriwa ni wachofu, wapo hoi bin taabani hao ndio wanaonyang’anywa bunduki,” alisema Lugola.
Amesema amelielekeza Jeshi la Polisi, wahakikishe kuwa Makampuni hayo yanaajiri askari ambao wanasifa za kufanya kazi hiyo, pamoja na wahakikishe wanaajiri askari wenye sifa na kuwalipa askari hao vizuri, kwa kuwa baadhi ya wamiliki wa kampuni hizo wamekua wakiwatapeli, kutokuwalipa, na wengine wanakopwa na ofisi zao.
“Askari gani wanakopwa, hawalipwi, huyo ni askari wa namna gani, matokeo yake askari huyo ambaye ana dhana ya moto anaweza kushawishika akafanya matumizi ya silaha ambayo hayaruhusiwi, au mali za wananchi zikaporwa kwasababu huyo ameshakata tamaa, kwahiyo niwatake makapuni yote ya ulinzi ambao askari wao watanilalamikia mimi au watamlalamikia Inspekta jenerali wa polisi kwamba hawalipa askari wao, hatuwezi kukubali kuwa na askari wanaofanya shughuli za ulinzi na usalama ndani ya nchi hii ambao hawalipwi, nitahakikisha makampuni hayo nitayachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha yanafutwa kwenye madaftari ya makampuni ya ulinzi nchini,” alisema Lugola.
Aidha, Waziri Lugola katika ziara anayoendelea nayo jimboni kwake, kwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, pamoja na kuchangia ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari, zahanati, pia aliwataka wananchi wa jimbo hilo, kufanya kazi kizaelendo kujenga miundombinu, na kutofikiria kazi za maendeleo zinafanywa na Serikali pekee.