Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika nyumba ya Bwana na Bibi Josam Paulo ikiwa ni ishara ya uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera, Julai 18, 2019. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka na wa wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
Sehemu ya umati wa wananchi wa kijiji cha Nyakabwera wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera, wakimsalimu Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kwa kuinua mikono, alipofika kuwawashia rasmi umeme na kuzungumza nao, akiwa katika ziara ya kazi Julai 18, 2019.
……………………
Na Veronica Simba – Kagera
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewasha rasmi umeme katika kijiji cha Nyakabwera wilayani Kyerwa na Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera, tukio lililoibua furaha kwa wakazi wa vijiji hivyo.
Akiwa amefuatana na viongozi na wataalamu mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa; Waziri aliwasha umeme katika maeneo hayo na kuzungumza na wananchi, akiwa katika ziara ya kazi, jana, Julai 18, 2019.
“Nampongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli; anafanya kazi kubwa. Katika sekta ya nishati, amedhamiria kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini,” Waziri Kalemani aliwaambia wananchi.
Kabla hajawasha rasmi umeme katika vijiji hivyo, Waziri alitoa hamasa kwa wananchi wa maeneo husika ambao hawajaunganishiwa umeme, kuchangamkia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kulipia gharama inayohitajika ambayo ni shilingi 27,000 ili wote wawe na umeme.
Vilevile, aliwataka kulinda miundombinu ya umeme iliyopo katika maeneo yao ili kuiwezesha serikali kuendelea kuwapatia huduma hiyo kwa ufanisi.
Alisema atakayebainika kuhujumu miundombinu hiyo, atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia, aliwashauri viongozi wa taasisi za umma pamoja na miradi mbalimbali ya kijamii kama vile mitambo ya maji, shule, vituo vya afya, masoko, nyumba za ibada na kadhalika, kutenga fedha za kulipia huduma ya kuunganishiwa umeme ili nishati hiyo ipelekwe katika maeneo hayo muhimu.
“Sambamba na hilo, viongozi ainisheni maeneo ambayo mmepanga kujenga miradi ya maendeleo na taasisi za umma ili mkandarasi ayapelekee umeme, ili muda wa kujenga utakapofika, kuwepo na nishati hiyo tayari,” alielekeza.
Aidha, Waziri alihamasisha matumizi ya vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) katika kuunganisha umeme ili kuepuka gharama kubwa za kutandaza mfumo wa nyaya za umeme kwenye majengo. Aligawa vifaa hivyo bure katika vijiji vyote viwili na kumtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini katika maeneo hayo kutowauzia wananchi vifaa hivyo hadi pale vilivyotolewa bure na serikali vitakapoisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa katika maeneo hayo, waliishukuru serikali kwa jitihada zake za kuwafikishia wananchi maendeleo kupitia uunganishaji umeme.
Waliomba maeneo yaliyosalia yafikishiwe huduma hiyo mapema ili wananchi wote wanufaike kwa kuanzisha biashara ndogondogo kwa ajili ya kuinua maisha yao kiuchumi.