NA MWAMVUA MWINYI,MAFIA
WILAYA ya Mafia ,mkoani Pwani imejipanga kuinua uchumi wake kwa kutumia zao la kibiashara la nazi na Mwani ambayo kwa sasa yananunuliwa kwa bei ya chini na kuwakandamiza wakulima wa mazao hayo.
Aidha halmashauri ya wilaya hiyo, imetoa jumla ya sh.milion 68.758 ikiwa ni mkopo kwa vijana ,wanawake na walemavu kwa mwaka 2018/2019.
Mkuu wa wilaya ya Mafia,Shaibu Nnduma akizungumza na madiwani pamoja na baadhi ya viongozi wa ofisi ya mkoa wa Pwani alieleza, fedha hizo ni mikopo ambayo watarudisha bila riba.
“Fedha hizo zimetokana na mapato ya ndani ya halmashauri ambapo imegawiwa kwa vikundi 12 kutoka kila kata zilizopo katika halmashauri hiyo”alifafanua Nnduma.
Hata hivyo Nnduma alisema, Mafia ni wilaya inayozalisha nazi kwa kiwango kikubwa tani 35,000 kila mwaka na kulikuwa hakuna kiwanda ila maamuzi ya kuanzisha kiwanda cha kusindika mafuta kitasaidia.
“Nazi zinauzwa hadi sh.100-150 na wakati mwingine zinaokotwa tuu chini hivyo uanzishaji wa kiwanda utainua soko hilo”alisisitiza Nnduma.
Akielezea zao la mwani alibainisha, Jibondo na Chole soko lipo Zanzibar na Dar es salaam wanauza bei chini sh 300 kwa kilo ,wakulima wanalalamika hivyo ukiwekwa mfumo mzuri wa kuiuza utaongeza pato la wakulima hao.
Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa wa Pwani ,(RAS)Theresia Mmbando aliipongeza halmashauri hiyo kwa kusimamia vyanzo vya mapato na kutenga asilimia zinazopaswa kusaidia wanawake,vijana na walemavu.
Theresia aliyataka makundi yanayopatiwa mkopo huo kuutumia vizuri kwa kuzalisha na sio kuingia tamaa ya kula hela ama kufanya matumizi mabaya ya fedha.